Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Primary Question
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza: - Je, ni lini Tarafa ya Enduimet pamoja na Vijiji vya ELerai, Tingatinga na Sinya vitaunganishwa na mradi wa maji kutoka Mto Simba hadi Longido ambao umepita katika maeneo hayo?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Lakini kabla ya maswali yangu niweke hii kumbukumbu kwa usahihi kabisa, kwamba kwanza nashukuru Serikali kwa kutupatia jamii ya Longido maji safi na salama kutoka Mto Simba ambayo mpaka sasa yamekuwa toshelevu katika Mji wa Longido ambako ni Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia kwa sababu kazi inaendelea kuelekea Kimokouwa, Eworendeke na Namanga, na ni mradi ambao bado haujakamilika. Nashukuru pia kwa kuwa imefika Engikaret, lakini bado hayajafikiwa Kiserian na baadhi ya maeneo yaliyokusudiwa kama kitongoji cha Wasinyai na Yambaluwa Yambalua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza la nyongeza. Kwa kuwa mradi huu bado una hayo mapungufu ya kufikisha maji katika maeneo hayo;
Je, ni lini Serikali itakwenda kukamilisha huo mradi wa kufikia maji maeneo yote yaliyolengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wananchi waliopitiwa na bomba hilo kutoka kule chanzo chake, waliopo kitongoji cha Emotong, ni kitongoji kikubwa sana ile scheme nyingine inayokwenda mpaka Larang’wa na Kamwanga haipitiki huko kabisa;
Je, ni lini watu wa Emotong, Tingatinga, a Engerian ambao nao waliahidiwa kwamba watapata matawi ya haya maji na bado hawajayapata watapata hayo maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami nipende kupokea shukrani zake kwa sababu amekiri kazi kubwa ambayo Wizara tumeendelea kufanya katika jimbo lake; na huo tu ni mwanzo wa mageuzi makubwa ambayo wizara inaendelea kuyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa miradi hii tunatarajia kadri pesa tunavyoendelea kupata, na mwaka ujao wa fedha tutaendelea kuhakikisha hii miradi inakamilika. Hii ni kwa sababu lengo la Wizara ni kuona kwamba miradi inakamilika na wananchi wanapata maji safi na salama ya kutosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitongoji cha Tingatinga na maeneo hayo mengine vilevile wao pia wapo kwenye Mpango Mkakati wa Wizara kuona nao wao pia wanakwenda kunufaka na maji safi na salama. Hivyo nikutoe hofu Mheshimiwa Mbunge kama ulivyoona kazi imeweza kufanyika kwenye maeneo mengine na maeneo haya pia kazi itakuja kufanyika na maji bombani yatapatikana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved