Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

George Ranwell Mwenisongole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE K.n.y. MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto ya msongamano wa magari yanayovuka kuelekea nchi jirani kupitia mpaka wa Tunduma?

Supplementary Question 1

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Spika, msongamano huu wa magari katika Mji wa Tuduma haujaathiri tu magari yanayopita mpakani, lakini umeathiri wananchi na usafiri wa daladala, na wananchi wote hata wanaokwenda mikoa ya jirani. Lakini Mheshimiwa Rais, Marehemu Dkt. Magufuli, alipofika wakati wa kampeni aliahidi kilometa 10 za lami kwa ajili ya kupunguza huu msongamano kwa ajili ya kujenga njia za pembezoni na za mchepuko. Sasa nini kauli ya Serikali kuhusu ahadi hii ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa ya kilometa kumi za lami ili kupunguza msongamano katika Mji wa Tunduma? Ahsante.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tunakubali kwamba ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais. Lakini kwa kutambua changamoto ya msongamano ambayo ipo pale Tunduma, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ina mambo yafuatayo ili kuondoa hizo changamoto za msongamano.

Mheshimiwa Spika, kwanza, tunategemea kubadilisha mfumo wa mizani iliyopo iwe ni weigh in motion ambayo inachukua muda mfupi sana, pale Mpemba ambayo ni jirani, kama kilometa 10 pale Tunduma, ambayo inachukua takribani dakika moja mpaka mbili gari linakuwa limeshapita. Kwa hiyo, itakuwa ni moja ya njia za kuondoa msongamano.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, nitumie Bunge hili kusema kwamba Halmashauri ya Tunduma waweze kuongeza maegesho ili magari ambayo hayaendi kwenye Kituo cha Forodha yasiwe na sababu ya kukaa barabarani. Kwa hiyo, ni fursa kwa Halmashauri ya Tunduma kuongeza maegesho.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa tatu, ile barabara sasa hivi tunaifanyia utaratibu tuweze kupanua njia ili kuwe na lane badala kuwa na lane mbili ziwe walau ziwe hata lane nne, lakini mkakati wa nne ni kutengeneza bypass ya barabara ili magari yote ambayo yanakwenda ama yanatoka yaani yanakwenda Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Katavi hadi Kigoma yasiwe na sababu ya kupita Tunduma, kwa hiyo yapite pembeni ili kuruhusu hii barabara sasa iwe huru na tunaamini tukifanya hivyo tutakuwa tumepunguza sana msongamano katika njia hii. Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Primary Question

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE K.n.y. MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto ya msongamano wa magari yanayovuka kuelekea nchi jirani kupitia mpaka wa Tunduma?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza kwenye suala hili la msingi lililolenga Wizara ya Fedha.

Katika mpaka wa Namanga kuna tatizo kubwa sawa la Tunduma la msongamano wa magari ambayo wakati mwingine huchukua hata zaidi ya siku tatu yakingojea kuwa cleared yaweze kuendelea na safari na adha kubwa inayotokea ni kwamba hakuna miundombinu ya vyoo, mahali pa kuoga wale wanaokaa kwenye malori na wanachafua sana mazingira.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inampango gani wa kuhakikisha kwamba wakati mipango ya kutengeneza maeneo sahihi ya kuengesha haya malori na sisi Longido tuna sehemu TANROADS wametenga zaidi ya hekari 200 na ujenzi unaendelea, wana mpango gani wa kuhakikisha kwamba wananchi wa mipakani hawapati magonjwa ya mlipuko kwa sababu ya msongamano wa magari na hakuna miundombinu ya kijamii?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa wa Jimbo la Longido kwamba Serikali inazifahamu hizo changamoto na tupo kusaidiana na wenzetu, sisi ndiyo tunaojenga vile vituo tunayatambua hayo na tutahakikisha katika mpango wa karibu tunakwenda kuondoa hizo changamoto ikiwa ni pamoja na kujenga hiyo miundombinu ya haraka ili wananchi wasiweze kupata adha ikiwa ni pamoja na kuangalia utaratibu wa kupunguza ile misongamano kwa kujenga barabara na maegesho makubwa ili magari yatakayokuwepo kwenye foleni ni yale tu ambayo yanatakiwa kwenda kwenye Vituo vya Forodha, ahsante.