Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. David Mathayo David
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Same Magharibi
Primary Question
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: - Wananchi wa Wilaya ya Same bado wanaendelea kutaabika sana kwa kukosa huduma bora za afya kwenye Hospitali ya Wilaya licha ya ahadi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ya ujenzi wa hospitali mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Same. Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa ikizingatiwa kuwa eneo la ujenzi wa hospitali hiyo tayari limeshatengwa?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kunipa nafasi hii lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kutupa majibu yenye matumaini kwa Jimbo la Same Magharibi na Wilaya nzima ya Same, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa hii ni ahadi ya Waziri Mkuu kujenga Hospitali ya Wilaya ya Same na kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Same ipo katika barabara kuu inayokwenda Arusha ambapo ajali nyingi sana zinatokea na watu wote wanaopata matatizo haya wanategemea kupata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Same na kwa kuwa eneo limeshatengwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Same.
Je, Serikali inapoanza kujenga hospitali mpya 43; Wilaya ya Same itapewa kipaumbele ili iweze kujengwa hospitali na kuletwa vifaa tiba pamoja na wafanyakazi wa kutosha?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Sera ya Serikali ni kuwa na zahanati angalau kwa kila kijiji na kituo cha afya kila kata; na kwa kuwa katika Jimbo langu tumejenga zahanati za kutosha takribani asilimia 80 lakini hatuna wafanyakazi na hatuna vitendea kazi.
Je, Serikali ni lini itapeleka watumishi wa afya kwenye zahanati hizo ili tuache kuzifunga zianze kutumika kusaidia wananchi wa Wilaya ya Same?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa David Mathayo David kwa juhudi zake za kuhakikisha mara kwa mara anawasiliana na Serikali kuhakikisha Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Same inajengwa; na mimi nimuhakikishie Serikali itaendelea kushirikiana naye lakini na wananchi wa Same kuhakikisha katika vipaumbele hivi tunakwenda kujenga Hospitali ya Wilaya ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, hii ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na kama ilivyo ada ahadi za viongozi wetu wa Kitaifa zinapewa kipaumbele; na mimi naomba nimuhakikishie kwamba Serikali tayari imeshaainisha ahadi zote za kitaifa za viongozi wetu wa kitaifa na zinakwenda kufanyiwa kazi kwa awamu na hospitali hii ya Same ikiwemo.
Mheshimiwa Spika, lakini pili, ni kweli tuna sera ya zahanati katika vijiji na vituo vya afya katika kata, lakini tumeamua kufanya mapitio ya sera ile ili tuwe na ujenzi wa zahanati kimkakati zaidi, lakini pia ujenzi wa vituo vya afya kimkakati zaidi badala ya kuwa kila kijiji na kila kata. Lakini nimhakikishie vituo hivi vyote ambayo vimejengwa Serikali inaendelea kuajiri na watumishi hao 2,726 walioajiriwa wapo ambao watapelekwa Same na katika awamu nyingine za ajira tutahakikisha tunapeleka watumishi Same. Ahsante.
Name
Jackson Gedion Kiswaga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Primary Question
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: - Wananchi wa Wilaya ya Same bado wanaendelea kutaabika sana kwa kukosa huduma bora za afya kwenye Hospitali ya Wilaya licha ya ahadi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ya ujenzi wa hospitali mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Same. Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa ikizingatiwa kuwa eneo la ujenzi wa hospitali hiyo tayari limeshatengwa?
Supplementary Question 2
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Kijiji cha Magulilwa, Kata ya Magulilwa, Jimbo la Kalenga walishamaliza boma la kituo cha afya siku nyingi sana; je, ni lini Serikali itatukamilishia ujenzi wa boma hilo? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, likiwemo boma hili la Magulilwa la kituo cha afya na maboma mengine yote ya vituo vya afya na zahanati, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumefanya tathmini na kuorodhesha maboma yote na mpaka tarehe 31 Mei, 2021 tulikuwa na jumla ya maboma 8,003 ambayo tunayapa kipaumbele cha kutenga fedha kwa awamu ili yakamilike. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba boma hili la Magulilwa litapewa kipaumbele. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved