Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Primary Question

MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:- Nachingwea ni miongoni mwa Wilaya chache zilizo na historia ndefu katika kusaidia nchi nyingi za Afrika kupata uhuru; kwani wapiganaji wengi wa nchi hizo walihifadhiwa kwenye Kambi ya Ukombozi Farm 17 iliyopo Nachingwea:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya Kambi ya Farm 17 hata kama yamegeuzwa kuwa Sekondari ili kuwa maeneo ya kihistoria na kuweza kuwavutia watalii? (b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzishawishi nchi zilizonufaika na Kambi ya Farm 17 kama Msumbiji na Zimbabwe ili ziangalie kwa karibu kambi hiyo kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu muhimu zilizopo?

Supplementary Question 1

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza;
Swali langu la kwanza ninataka tu nipate ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, hii project ya Road to Independence, nimepitia bajeti zote za Wizara ya Ulinzi, nimepitia bajeti ya Wizara ya Utamaduni, sijajua kama anaweza akaweleza wananchi wa Nachingwea ni kipindi gani haswa inaenda kutekelezwa hii program ili tuweze kujua kwa sababu miundombinu ya eneo lile bado inaendelea kuharibika mpaka sasa hivi tunavyozungumza, ikiwemo eneo ambalo ameisha Mheshimiwa Samora Machel.
Swali la pili ambalo ninapenda kuuliza, ni nini kazi za Mabalozi wetu katika nchi hizi ambazo zilinufaika na maeneo haya, ukienda Msumbiji leo hii kuna Chuo Kikuu kinaitwa Nachingwea University kinapatikana pale Msumbiji. Je, hawaoni umuhimu wa kushirikisha Balozi zetu na nchi zilizohusika kuweza kusaidia maeneo haya ili kuweza kuweka kumbukumbu za Viongozi ambao waliishi katika maeneo haya? Ahsante.

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza nitatoa utangulizi kwamba historia ya ukombozi wa Bara la Afrika haiwezi kutenganishwa na ushiriki mahiri na wa kujitoa wa nchi yetu Tanzania. Haiwezi kutenganishwa na uwepo wa Viongozi mashuhuri kama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini pia na Viongozi wengine wa Bara la Afrika kama kina Nkwame Nkurumah na hao wapiganaji wenyewe wakina Samora Machel wakina Robert Mugabe na wengine. Kwa maana hiyo, hii historia japokuwa ni chungu na japokuwa ni ngumu hatuna sababu ya kusema tunaweza tukadharau kutunza maeneo ambayo historia hiyo inayathamini, kwa maana hiyo eneo hili la Nachingwea ambalo Mheshimiwa Mbunge analizungumzia litapewa kipaumbele kwenye program hiyo ya Road to Independence ambayo nimeizungumzia hapa. Program hii kama anavyosema kwenye bajeti haionekani, naomba mimi na yeye tushirikiane kwa pamoja baada ya kikao hiki cha Bunge kufanya utafiti kwenye vitabu vya bajeti ili tuone ni wapi haswa bajeti hii ya Road to Independence inapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana usiwe mradi ambao unatokana na bajeti ya ndani ukawa ni mradi ambao pengine una ushirika wa hawa wabia anaowasema wakiwemo wafadhili wa maendeleo ama Vyuo Vikuu ambavyo vinapenda kufuatilia historia ya ukombozi wa Bara la Afrika.
Swali la pili, kwamba hatuoni kama Balozi zetu zinaweza zikashirika nchi hizo, Tanzania tulikuwa na jukumu kubwa tu ambao tulijitolea kulibeba la kutafuta ukombozi wa Bara la Afrika na kuwapa nyumba na makazi, mafunzo, chakula na malazi zaidi ya wapiganaji kutoka nchi zaidi ya 12 za Afrika zilizokuwa zinapambana na ukoloni na kwa maana hiyo, hiyo ni heshima ya kipekee ambayo sisi tuliipata kupata wapiganaji wa ukombozi kwenye nchi zao kuja kukaa katika nchi yetu. Heshima hiyo tunaendelea kuipata leo na mwaka jana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitunukiwa heshima ya kipekee pale AU kwa kupewa jengo la Peace and Security katika Mkutano wa Marais wa Afrika na hivi tunavyoongea hapa katika watu watatu mashuhuri wa Bara la Afrika ambao wanatambuliwa na wamewekewa alama za kipekee pale Addis Abba kwenye Makao Makuu ya AU ni pamoja na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wengine wakiwa ni Nkwame Nkurumah na mwingine akiwa ni Nelson Mandela.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, Tanzania itaendelea kuwapokea na kuwapa ushirikiano wapiganaji wote ambao wanapenda kuja Tanzania kwenye maeneo waliyowahi kuishi kama vile kufanya hija na kukumbukia siku ambazo walikuwepo hapa nchini wakipigania uhuru wa nchi zao, ambazo sasa zimekuwa huru.