Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itasaidia na kufanikisha kutoa namba kwa Vijiji vya Chipunda Kata ya Namatutwe, Mkalinga Kata ya Chikunja na Sululu ya Leo Kata ya Namatutwe vyenye Wakazi zaidi ya elfu kumi katika Jimbo la Ndanda?
Supplementary Question 1
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, majibu ya Serikali ni mazuri hata hivyo majibu haya yanatofautiana na majibu ambayo Serikali hii ilijibu mwaka 2016. Wakati huo walisema kwamba wamesimamisha kutoa namba za maeneo ya utawala mpaka pale watakapokamilisha taratibu zote kwa maana ya kupata watendaji, ofisi na mahitaji muhimu ili kuweza kuwa na vijiji. Leo Serikali inasema kwamba endapo watakamilisha taratibu hizi ambazo zilishakamilika zaidi ya miaka kumi, sasa swali langu kwa je, endapo nitaleta hizo documents zote zinazotoka kwenye Halmashauri ya Wilaya Masasi, Serikali itachukua muda gani kuhakikisha namba za vijiji hivi zinatolewa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi katika maeneo mbalimbali kwa sababu Serikali imekuwa inatoa namba lakini baadaye maeneo mengine yanatangazwa kuwa ni hifadhi, maeneo mengine ni mipaka kati majeshi pamoja na vijiji mfano Kijiji cha Chingulungulu ambapo kuna Hifadhi ya Misinjesi lakini Kijiji cha Ngalole ambapo wanapakana na Magereza ya Namajani, Wilaya ya Masasi. Vijiji hivi vyote vina namba na Serikali ipo pale inasema kwamba na yenyewe pia ni maeneo yao.
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya taasisi hizi kujiridhisha kwanza kabla ya kuamua kutwaa maeneo haya ili waweze kuwalipa fidia ama yachukuliwe na Serikali? (Makofi)
Swali la pili; kulikuwa na migogoro mingi katika maeneo mbalimbali ya ardhi, kwa sababu Serikali imekuwa inatoa namba lakini baadaye maeneo mengine yanatangazwa kuwa ni hifadhi na mengine ni mipaka kati ya majeshi pamoja na vijiji, kwa mfano Kijiji cha Chingulungulu ambapo kuna Hifadhi ya Misinjesi na Kijiji cha Ngalole ambako wanapakana na Magereza ya Namajani Wilaya ya Masasi; vijiji hivi vyote vina namba na Serikali iko pale inasema kwamba na yenyewe pia ni maeneo yao.
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya taasisi hizi kujiridhisha kwanza kabla ya kutwaa maeneo haya ili waweze kuwalipa fidia kabla ama yachukuliwe na Serikali?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, kwamba Serikali kwa kipindi kile cha mwaka 2016 kilikuwa kinafanya mapitio ya kukamilisha mfumo bora zaidi wa usajili wa maeneo mapya ya utawala. Kwa hiyo, tangazo na maelekezo yale ya Serikali yalikuwa sahihi na yalifanyika kwa wakati ule na ndiYo maana leo Serikali imetoa maelekezo kwamba sasa Halmashauri ya Ndanda pia tunaweza tukaanza utaratibu wa kusajili vijiji hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba akileta documents zinazohitajika, tutapitia taratibu husika na muda siyo mrefu sana, baada ya mamlaka kujiridhisha uhalali na vigezo vya vijiji vile, basi tutapata vijiji vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, mahusiano ya usajili wa vijiji; ili kiwe Kijiji ni lazima kipate Hati ambayo inatolewa na TAMISEMI. Hivi sasa vijiji vilivyosajiliwa kwa record yangu havipungui 12,319. Baada ya hapo kila Kijiji kinatakiwa kipate Cheti kutoka kwa Kamishna wa Ardhi ili kuonyesha mipaka ya Kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila Kijiji Tanzania lazima kiwe na vyeti viwili; Hati ya kusajiliwa, ni Mamlaka ya Utawala kwamba sasa mnaweza kuchaguana, ni Serikali kamili. Baada ya hapo inatakiwa Kijiji kipimwe ili kiweze kupata Hati, yaani Cheti kinachoonyesha sasa utawala wenu wa Serikali unamiliki ardhi kiasi gani. Kwa hiyo, hivi sasa kuna vijiji 1,557 ambavyo havijapata Hati au Vyeti vile vya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nahisi namna ya kuondoa mgogoro huu wa Ndanda, kwanza ipatikane hiyo Hati ya kusajili Kijiji, halafu tukapime mipaka ya Kijiji kile. Siyo kweli kwamba Kijiji hakiwezi kuwa na msitu, kinaweza kuwa na msitu, lakini Cheti chenye heshima na kinachothaminiwa na kinachotakiwa kisheria ndani ya Kijiji ni Cheti cha umiliki wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba Waheshimiwa Wabunge, tushirikiane kuhakiki kwenye vijiji vyetu kuhakikisha kila Kijiji kina vyeti viwili; kwanza, wana Hati ya kusajiliwa kama Serikali na pia vyeti vya kumiliki ardhi. Sasa ndani ya Kijiji kunaweza kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi unaoonyesha misitu, makazi, kilimo na ufugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kuongeza hilo, sikuwa namjibia Waziri wa Maliasili, lakini nilikuwa natoa ufafanuzi kwamba kila kijiji kinatakiwa kipimwe kipewe Cheti cha Ardhi ya Kijiji. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Sawa. Mheshimiwa Waziri, tunakushukuru kwa huo ufafanuzi. Nadhani hoja ya msingi ni kwamba Kijiji kinapopewa Hati lazima kuna vigezo ambavyo inatakiwa iwe navyo, ikiwa ni pamoja na ardhi na idadi ya watu. Kwa hiyo, Maliasili sasa wakienda pale, ile ardhi ambayo inajulikana ni ya Kijiji, halafu wao wakaweka hifadhi hapo, halafu na nyie mkaja mkakipunguza ukubwa kile Kijiji, nani anakuwa amekuja kwanza kabla ya hapo? Aliyemtangulia mwenzie ni nani? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Maliasili hawawezi kupora ardhi kwenye vijiji, hawawezi. Kwanza Maliasili hawatoi Cheti, wala hawatoi Hati. Wao wanatengeneza GN. Msitu wa Maliasili unaweza kuwa sehemu ya ardhi ya Kijiji. Kikubwa hapa ni Hati; Cheti kinachotawala ardhi ya Kijiji, lakini ndani mle kunaweza kuwa na shughuli mbalimbali hata za kibinadamu ndani ya Kijiji.
NAIBU SPIKA: Sawa, ahsante.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, mnaweza kuwa na ardhi ya Serikali au ya watu binafsi ndani ya Kijiji, lakini Cheti cha Kijiji kinaonyesha mipaka ya utawala ya Kijiji kizima pamoja na ardhi iliyopo.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved