Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Francis Kumba Ndulane

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kaskazini

Primary Question

MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: - Je, ni lini barabara ya Nangurukuru – Liwale yenye kilometa 258 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 25 inavyoelekeza?

Supplementary Question 1

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza, napenda kumwuliza Waziri wa Ujenzi kwamba, kwa kuwa katika mwaka 2019, Serikali ilichepusha katika Kijiji cha Njinjo, barabara ya Nangurukuru – Liwale na hivyo ililazimu kulipa fidia kwa baadhi ya wananchi ambao walikuwa na mali zao katika lile eneo ambalo limechepushwa barabara; lakini kuna wananchi wawili hadi kufikia sasa hawajalipwa fidia ya mali zao; nao ni Mama Mary Mahmoud Kiroboto pamoja na Ndugu Said Salum Karanje, ambao wanadai jumla ya shilingi 13,264,180/ =. Napenda kujua: Je, Serikali ni lini itawalipa wananchi hawa wawili haki yao ya fidia kwa ajili ya kuchepusha kipande kile cha barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, napenda kumwuliza Waziri kwamba, kwa kuwa wakati wa maadhimisho ya Kumbukizi za Vita vya Majimaji ilipotimiza miaka 100 mwaka 2010, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati ule, aliwaelekeza Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Lindi…

NAIBU SPIKA: Uliza swali lako, Mheshimiwa Ndulane.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nashukuru. Alitoa maelekezo wafungue barabara kati ya Nandete na Nyamwage: Je, mpango huu umefikia wapi wa kufungua barabara ile ya kipande cha Nyamwage kwenda Nandete? Ahsante. (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa, Francis Ndulane Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake amesema kwamba, kulitolewa ahadi na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tatu. Napenda tu nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa hii barabara ilitakiwa ifunguliwe maana yake haipo kwenye mtandao wa barabara za TANROAD wala za TARURA. Hivyo napenda nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imelichukua na tutawasiliana na Meneja wa TANROAD Mkoa wa Lindi ili tuweze kupata taarifa sahihi na ahadi hii ili tuweze kuanza kuitekeleza ama kama ilikwama tujue ni kwa nini ilikwama wakati ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili, kama ulivyotoa maelekezo, ni swali ambalo lipo very specific na kama watu hao wapo ni bora wakaandika barua rasmi kwa TANROAD Mkoa wa Lindi, wakupe copy na sisi watupe copy ili tuweze kuliangalia, kwa sababu ni suala la watu wawili, tuweze kuliangalia kama lina changamoto gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Daimu Iddi Mpakate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Primary Question

MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: - Je, ni lini barabara ya Nangurukuru – Liwale yenye kilometa 258 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 25 inavyoelekeza?

Supplementary Question 2

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Changamoto iliyopo kwenye barabara ya Liwale -Nangurukuru inafanana kabisa na changamoto iliyopo kwenye barabara ya Mtwara Pachani, Lusewa kwenda Nalasi mpaka Tunduru Mjini. Mwaka, 2015 aliyekuwa mgombea mwenza ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, alitoa ahadi barabara ile kutengenezwa kwa kiwango cha lami. Nashukuru Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu mwaka jana 2020: Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI – (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mtwara - Pachani hadi Nalasi ni barabara ambayo tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa hiyo, kinachosubiriwa sasa hivi ni Serikali kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga hii barabara. Kwa hiyo, tayari taratibu zimeshaanza, tunachosubiri tu ni fedha ipatikane. Katika Awamu hii ya miaka mitano, kama fedha itapatikana, basi itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kutekeleza hiyo ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: - Je, ni lini barabara ya Nangurukuru – Liwale yenye kilometa 258 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 25 inavyoelekeza?

Supplementary Question 3

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu. Barabara ya Nangurukuru - Niwale ni mwaka wa tano inatengwa fedha kwa ajili upembuzi yakinifu na usanifu wa kina…

NAIBU SPIKA: Uliza swali. Taja barabara unayotaka ijibiwe.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Nangurukuru - Liwale, fedha hazijawahi kuletwa tangu zinatengwa miaka yote mitano.

NAIBU SPIKA: Swali lako ni nini?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali italeta fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya Nangurukuru - Liwale? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, swali la nyongeza la mheshiiwa Kuchauko ndiyo lilikuwa swali la msingi na Serikali imetenda shilingi milioni 548.603 na tumesema taratibu zote zimekamilika na muda wowote inatangazwa.