Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Hifadhi ya Taifa Mkomazi imebana sana maeneo ya wananchi na kusababisha kazi za kijamii katika Kata za Lunguza, Mng’aro na Mnazi kushindwa kufanyika: - Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kupunguza sehemu ya Hifadhi ya Mkomazi na kugawa kwa Serikali za Vijiji?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ambayo siyo ya matumaini sana kwa wananchi wa Tarafa ya Umba, hasa Kata ya Mnazi na Lunguza, tunayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa shughuli za wananchi hawa wanaozungukwa na hifadhi ya Taifa Mkomazi sehemu yao kubwa ni ufugaji na eneo lao ni dogo, lakini uanzishwaji wa hifadhi haujawatendea haki kwa sababu hakuna mlango hata mmoja wa kuingilia hifadhini kutokea upande huu wa Lushoto.

Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga geti la kuingia Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi katika eneo la Kamakota, Kijiji cha Kivingo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa ukaribu huu wa Hifadhi na makazi ya watu unasababisha mara kwa mara wanyama waharibifu, hasa tembo, kuvamia mashamba katika Vijiji vya Mkundo- Mbaru, Mkundi-Mtae, kiasi kwamba zaidi ya ekari 3,000 za matikiti maji na mkonge zimeharibiwa vibaya na tembo.

Je, Waziri yuko tayari sasa kuwatembelea wananchi wale ili angalau akawaone na kuweza kuwafariji?

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Shangazi kwa kuendelea kuhamasisha utalii, hasa katika maeneo ya Jimbo lake la Mlalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu Wilaya ya Lushoto ni eneo moja wapo ambalo linasaidia sana kuongeza mapato ya Serikali, hasa kisekta, na Mheshimiwa Shangazi amekuwa mara nyingi akitutembelea katika ofisi zetu kuelezea changamoto za maeneo hayo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba Serikali inatambua mchango wkae, lakini pia tuko bega kwa bega kuhakikisha kwamba utalii unasonga mbele, ikiwemo eneo hili la Mlalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ameomba kuhusu kuweka geti katika eneo la Kamakota, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti hii ambayo mmetupitishia, geti hili litafunguliwa ili kurahisisha watalii wanaoelekea maeneo ya Lushoto, hususan Mlalo, basi iwe rahisi sana kupita katika eneo hili la Kamakota.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utalii tutaufungua katika eneo hilo na tuna uhakika kwamba tutaweza kupata mapato mengi yanayotokana na Hifadhi yetu hii ya Mkomazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ameuliza kama Waziri yuko tayari; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafika Mlalo, kama siyo basi atakuwa ni Waziri, kuongea na wananchi na kuendelea kuwapa pole hata wananchi wengine wenye maeneo ambayo wanakutana na changamoto hizi za wanyama wakali na waharibifu kama tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.