Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Anastazia James Wambura
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: - Je, ni kwa kiasi gani suala la kuwapatia wazee wasiojiweza vitambulisho kwa ajili ya kupata matibabu bure limetekelezwa kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi?
Supplementary Question 1
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na kutokana na hayo basi swali langu la kwanza litakuwa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu zake na kwa jinsi hali halisi ilivyo, zipo Halmashauri ambazo hazijakamilisha zoezi hili na ni kwa madai kwamba hazina mapato ya kutosha. Sasa je, Serikali inatoa tamko gani kwa zile Halmashauri ambazo hazina fedha za kutosha kukamilisha zoezi la utambuzi na la utoaji vitambulisho? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba lipo tatizo wazee wanapofika hospitalini wanaandikiwa dawa na kuambiwa waende kununua katika maduka ya dawa kwa madai kwamba katika kituo husika hakuna dawa: Je, Serikali inatoa maelezo gani pale ambapo wazee wanakuwa wakiambiwa wakanunue dawa ilhali wanastahili kupata matibabu ya bure? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge Anastazia kwa kuendelea kuwatetea na kuwapambania wazee. Naomba kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kweli zipo Halmashauri ambazo zinashindwa kutimiza hili, kati yake zipo ambazo hawatimizi tu mpaka uwafuatilie sana na wapo wengine ambao kwa kweli uwezo wao unakuwa mdogo sana. Niseme kwenye bajeti yetu hii iliyopita, nilishukuru sana Bunge lako Tukufu kwa kupitisha ile bajeti yetu ya shilingi bilioni 149 ambazo tunatarajia kwenye muswada huu wa sheria zitakwenda kuhudumia zile nyumba zote wakiwemo wazee ambao watakuwa wamebainika kwamba hawana uwezo kabisa. Kwa hiyo, tunatarajia kumaliza kabisa hili suala la wazee hawa wasio na uwezo kabisa ili wawe covered kupitia Mpango wetu wa Bima ya Afya Kwa Wote tunaotarajia kwenda kuuchukua.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi tumekuwa na vikao vya kwenye mtandao pamoja na Mtandao wa Wazee nchi nzima, kila Jumamosi; tumeanza hiyo sera, “Jumamosi Zungumza na Wazee.” Tunafanya hivi vikao kujadili hizi changamoto. Wiki iliyopita tumekubaliana kwamba; awali iliagizwa asilimia sita ya bajeti tunayopanga lazima dawa zake ziende kwa wazee. Kwa hiyo, hata sasa hivi Serikali imefanya uamuzi wa kurudisha kupitia Hazina ile fedha ya Hospitali kwa mfano za Mikoa iliyokuwa inaenda moja kwa moja MSD, ili dawa zinapokosekana, zinunuliwe huko kwenye hospitali. Asilimia sita ya ile fedha ndiyo itumike kununua hizo dawa za wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Kamati za Maamuzi kwenye Vikao vya Bodi za hizi hospitali zetu, tumeona kwamba tuweke hata mwakilishi wa wazee awe anahakikisha kwamba anatetea ile hoja yake pale. Hii ni mikakati ya kufanya kwamba wazee wawe na sauti katika vikao vya maamuzi vya management za hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tumeanza mkakati wa kila hospitali; mnawaona wale wamevaa nguo za “Mpishe Mzee Apate Huduma Kwanza.” Hawa nao wanachukua takwimu za kujua mzee gani amekwenda kituoni, ameondoka bila dawa ili Medical Officer in Charge ahusike kuhakikisha mzee huyu anapata dawa kwa taratibu hizi za kuweka bajeti ya dawa pembeni yao. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved