Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Godwin Emmanuel Kunambi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Primary Question
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya mashamba pori yasiyoendelezwa Mkoani Morogoro?
Supplementary Question 1
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; ni lini Serikali itatatua mgogoro wa Shamba la Balali lenye ekari 2,000? Kwa sasa shamba lile yapata takribani miaka 20 Balali hajaliendeleza na wananchi wamekuwa wakilima humo. Ni lini sasa Serikali itafuta hati ya Balali na umiliki ule kupewa wananchi wa Jimbo la Mlimba, Kata ya Chita, pale Melela?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini Serikali itatatua mgogoro wa Shamba la Kambenga? Ahsante.
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba marehemu Balali alikuwa anamiliki, sasa hivi msimamizi wa mirathi ambaye ni mke wake anamiliki shamba hilo alilolisema na nafahamu kwamba halijaendelezwa. Hata hivyo, Serikali ilifanya jitihada za kumtafuta yule mwekezaji na kumpa notisi, akajieleza, lakini bado tulichukua hatua ya kutaka kuchukua sehemu ya shamba hilo ili wananchi waweze kunufaika na yeye kumpa mpango wa muda mfupi aweze kuliendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya wakati wa kupima hilo shamba wananchi hawakuelezwa vizuri, walifikiri wale wapimaji wanakwenda kumsaidia yule mwenye shamba wakachoma vifaa na magari yaliyokuwa yanatumika kwa kazi ile ya Wilaya ya Kilombero, ni bahati mbaya sana. Kwa hiyo tunachukua hatua nyingine, nimeelekeza kule kwamba sasa tutapeleka notisi ya kumwomba huyu mwenye shamba ajieleze, lakini pia tunafikiria namna ya mwenye shamba kuweza kulipa fidia ya vifaa na mali zilizopotea katika kutekeleza jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili jambo nalifahamu vizuri na nikiwa nje nitamweleza mengine ambayo yalisababisha hili, lakini kwa hapa itoshe tu kwamba Serikali inalitambua na tunachukua hatua juu ya shamba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; Shamba la Kambenga lilikuwa na mgogoro na vijiji na bahati mbaya sana mkuu wa mkoa aliyepita aliunda timu. Wizara yangu ilitaka kuingilia lakini Mkuu aa Mkoa mpya aliyekuja ameniomba muda kidogo atafsiri ile taarifa ya Kamati aliyoiunda mwenzake. Baada ya taarifa hiyo tutaamua, nilishaamua kumpeleka Kamishna kule, lakini nilisitisha kidogo baada ya maombi ya Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo yote haya mawili nayajua, yako ndani ya uwezo wa Wizara. Naomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kukumbushana tutayashughulikia haya yote mawili.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved