Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, ni lini wananchi wa Kata Saba za Tarafa ya Chamriho watapatiwa maji kutoka mradi wa maji ya Ziwa Victoria?
Supplementary Question 1
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali nimeyaona lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria ulioanza mwaka 2005 ukamalizika mwaka 2018, ambao ulikuwa unatoa maji Ziwa Victoria kuleta Bunda Mjini, na kwa kuwa mradi huo ulikuwa umejumuisha vijiji 30 ambavyo leo tunaviuliza hapa, na kwa kuwa bajeti ya mwaka 2020/2022 imeonyesha kwamba Jimbo la Bunda Vijijini litapewa maji ya Ziwa Victoria kutokea Bunda Mjini. Swali la msingi hapa ni lini sasa Waziri wa Maji ataenda Jimbo la Bunda Vijijini kutangaza mradi huu ambao ameugusia kwenye bajeti ya 2021/2022? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imetumia milioni 40 kufanya utafiti wa vijiji sita ambavyo vina uhaba wa maji kwenye maeneo hayo na maeneo hayo ni Mihingo, Tingirima, Rakana, Jaburundu, Salama A, Kambubu. Serikali imetumia milioni 40 kutengeneza tathmini ya mkakati wa kuchimba na makinga maji kama malambo ya maji hayo. Ni lini sasa itaenda kukamilisha mradi huo ambao uko hapo? (Makofi)
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Getere kwa ufuatiliaji wa karibu sana na kwa namna ambavyo tumeendelea kushirikiana naye. Nipende kumuambia tu Mheshimiwa Getere kwamba, suala hili la Bunda kuweza kutumia maji ya Ziwa Victoria ni suala ambalo ni la kimkakati Kiwizara na tunafahamu maji yameshafika pale Bunda Mjini na kwa eneo lake la Bunda Vijijini, Serikali ipo katika mkakati wa kuona kwamba mipango yetu ya muda mrefu inakwenda kufanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, na baada ya Bunge hili Wizara itatuma wataalamu pale kwenda kuangalia uwezekano wa kutumia yale maji yaliyofika Bunda Mjini na ikishindikana, basi watafanya review mpya kabisa kuona kwamba sasa maji kutoka Ziwa Victoria yanafika Bunda Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na swali lake la pili la kuhusiana na malambo sita ni kweli, Serikali tulipeleka milioni 40 na malambo yale tutakwenda kuyajenga awamu kwa awamu. Tayari lambo la kwanza lipo kwenye utekelezaji asilimia 40 lakini shughuli za ukamilishaji wa lambo hili, utaendelea baada ya mgao ujao wizara kupeleka fedha na kuhakikisha malambo yote sita kila tunavyopata fedha tutapeleka ili yaweze kukamilika. (Makofi)
Name
Robert Chacha Maboto
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: - Je, ni lini wananchi wa Kata Saba za Tarafa ya Chamriho watapatiwa maji kutoka mradi wa maji ya Ziwa Victoria?
Supplementary Question 2
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Mradi wa maji Bunda Mjini ulikuwa wa thamani ya shilingi 10,600,000,000 fedha zilizokwisha kutolewa mpaka sasa ni shilingi 2,600,000,000 bado shilingi bilioni nane. Je, ni lini Serikali itamalizia fedha hizi ili mradi ule uweze kukamilika? (Makofi)
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maboto kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mradi ule umeweza kupelekewa fedha hizi shilingi bilioni 2.6 na bado hizo shilingi bilioni 8 na fedha hizi tayari zipo kwenye mpango wa Wizara kuona kwamba tunaendelea kupeleka fedha. Ili kuweza kukamilisha mradi ule na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ameendelea kuifanikisha Wizara ya Maji, kwa kuongeza fedha tofauti na namna ambavyo tulipitisha kwenye bajeti yetu. Hivyo, mradi kama huu na wenyewe pia tunaupa jicho la kipekee kabisa kuhakikisha kwamba unakwenda kukamilika. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved