Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Omari Mohamed Kigua
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi?
Supplementary Question 1
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Binafsi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa uamuzi wa busara sana sana wa kununua magari katika halmashauri zote za Tanzania yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; ni ukweli usiopingika kwamba huduma ya ambulance ni muhimu sana katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania. Hata hivyo, huko nyuma imejitokeza changamoto kwamba huduma ya magari haya ya ambulance yanapelekwa sehemu moja mawili, matatu wakati sehemu nyingine hakuna magari kabisa. Sasa nini mpango wa Serikali katika kuepuka hili siku za usoni? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali imefanya jambo jema sana, inaenda kujenga vituo vya afya kwenye tarafa takribani nchi nzima. Je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tarafa zote hizo pia zinapata magari ya wagonjwa kwa maana ya ambulance? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nipokee shukrani nyingi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitoa kwa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na ni kweli Dhahiri, shahiri inaonyesha kazi kubwa sana ambayo Serikali yetu ya Awamu ya Sita inaifanya katika kuboresha huduma za afya katika nchi yetu kwa kasi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumekuwa tunapeleka magari ya wagonjwa katika halmashauri mbalimbali, lakini kuna vigezo ambavyo vimekuwa vikizingatiwa wakati tunapeleka magari na ndiyo maana kumekuwa na utofauti kidogo wa idadi ya magari yanayopelekwa kwenye halmashauri moja ikilinganishwa na magari yanayopelekwa kwenye halmashauri nyingine. Moja ya vigezo ni pamoja na idadi ya wananchi, wingi wa vituo vya afya, lakini pia idadi ya matukio ya magonjwa mlipuko, lakini na ajali za barabarani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utaratibu huu ni wa kisera tutaendelea kufanya hivyo, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha halmashauri zetu zote zinapata magari ya wagonjwa angalau kutimiza majukumu hayo bila kujali wingi wa wagonjwa na kadhalika, kwa maana ya kuhakikisha kwamba huduma zinapatikana vizuri. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge jambo hili tunalizingatia na mipango yetu ni kuendelea kuboresha.
Mheshimiwa Spika, la pili, katika ujenzi wa vituo vya afya katika kila tarafa; tunahitaji kuwa na vituo vya afya vyenye magari ya wagonjwa na magari haya yataendelea kuwekwa kwenye mipango na kufikishwa kwenye vituo vya afya vinavyojengwa katika tarafa zetu kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Pia kama nilivyotoa taarifa hapa, tuna magari mengi ya wagonjwa yanakwenda kununuliwa mwaka huu wa fedha na hivyo tutaendelea kuboresha utaratibu huo kufikisha magari hayo. Nakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved