Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto ya maji katika Jimbo la Nkasi Kaskazini?
Supplementary Question 1
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi, nami niulize maswali mawili ya nyongeza. Kabla sijauliza, tunafungwa sana na Sheria ya Takwimu, lakini naomba Bunge lako Tukufu, sheria hii isiwe ni kichaka cha kutoa takwimu za uongo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri anasema upatikanaji wa maji ni asilimia 52, wakati nafika hapa Meneja ananijibu ni asilimia 27. Sijui nani mkweli kati ya hizo taarifa? Nakosa maneno ya kusema kwa sababu ya Sheria ya Takwimu kwa sababu mtaniambia nimefanya research kupitia nini?
Mheshimiwa Spika, na mimi naomba kusema kwa sababu kwa miradi hiyo…
SPIKA: Hapa Bungeni unaruhusiwa, wewe sema tu, mradi usidanganye tu.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, Wana- Nkasi wanasikia, akisema asilimia 52, wakati Kata zenye uhakika wa kupata maji hazizidi mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kuna miradi miwili ambayo ni miradi kichefukichefu; Mradi wa Isale na Mradi wa Namanyere ambao una zaidi wa miaka mitatu; na miradi hiyo hata ikikamilika haiwezi kabisa kutatua changamoto ya maji Jimbo la Nkasi Kaskazini: Serikali haioni sasa kuna haja ya kuchukua Maji Ziwa Tanganyika ambayo ni kilometa 64 tu kuweza kumaliza changamoto ya maji? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kwa kuwa Serikali imepata huo mkopo ambao imegawa kwenye Wizara za Kisekta ikiwepo Wizara ya Maji, napenda kujua, Jimbo la Nkasi Kaskazini tunapata kiasi gani ili angalau ikapunguze makali ya changamoto za maji? (Makofi)
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Joseph Khenani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Dada yangu, Mheshimiwa Aida, kwa ufuatiliaji wa suala hili la miradi hii ya maji na nipende kukuhakikishia Mheshimiwa Aida kwamba miradi hii ambayo umeiita kichefuchefu tayari Wizara tumeipa nguvu na tutaisimamia kwa karibu sana kuona kwamba inakamilika. Kwa sababu lengo la Mheshimiwa Rais ni kumtua ndoo Mama kichwani nasi kama Wizara ya Maji ni wanufaika wakubwa wa fedha kutoka Serikali Kuu, hivyo, nikutoe hofu, nikuhakikishie tutasimamia na miradi hii itakamilika kama ambavyo miradi mingine mingi zaidi ya 200 ilivyoweza kukamilika.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu kuhusu fedha za Covid. Katika Jimbo la Nkasi Kaskazini pia wamekuwa wanufaika wa hizi fedha ambazo Mheshimiwa Rais ameweza kuzipigania. Tumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa sababu wananchi wa Nkasi Kaskazini na wao wametengewa milioni 500 kwa lengo la kufanya mradi wa Mpata.
Mheshimiwa Spika, lengo la hizi fedha ni kufanya mradi utakaokamilika ndani ya miezi sita, miezi tisa, uweze kutoa maji na wananchi wanufaike. Hivyo, tumeweza kuweka mradi mfupi ambao ndani ya shilingi milioni 500 utakamilika na wananchi watanufaika moja kwa moja. Kwa miradi hiyo ya Namanyere tayari ipo ina bajeti, kama Namanyere ina bilioni 1.5. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge nitaendelea kukupa ushirikiano kama ambavyo tumekuwa tukiwasiliana. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Halima James Mdee
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto ya maji katika Jimbo la Nkasi Kaskazini?
Supplementary Question 2
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani sasa hivi tunavyozungumza ambayo inahudumiwa na mitambo ya Ruvu Chini, nazungumzia Bagamoyo, nakuja Jimbo langu la Kawe pale, nakwenda Kinondoni, Temeke, kuna uhaba mkubwa sana wa maji.
Mheshimiwa Spika, Serikali inasema kwa sababu kuna upungufu wa maji, yaani kina cha maji kimepungua. Sasa ninataka Serikali iniambie, kwa sababu kupungua kwa maji kwa vyovyote vile kuna uhusiano na mabadiliko ya tabianchi, dunia nzima sasa hivi inazungumzia climate change. Leo nimemsikiliza Rais anasema anataka Serikali mtenge fedha za climate change.
Mheshimiwa Spika, nataka nipate majibu sahihi ili tatizo hili lisiwe la kudumu, kuna mkakati gani wa muda mfupi na muda mrefu kuweza kukabiliana na upungufu huu wa maji ili wananchi wa maeneo husika waepukane na kero hii? Hasa kwa kuzingatia miradi husika tumejenga kwa fedha za mikopo za mabilioni ya shilingi ambayo Taifa linalipa sasa hivi. (Makofi)
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli mitambo yetu ya Ruvu Chini hapa katikati ilipata hitilafu ya kupata maji kwa upungufu lakini kama Wizara tuna mabonde tisa ambayo yanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana kuona kwamba tunadhibiti tatizo hili. Tatizo hili ni kwamba matumizi ya shughuli za kibinadamu kwa sehemu kubwa ndiyo yameathiri.
Mheshimiwa Spika, huwa tunatoa vibali kwa wenzetu kufanya umwagiliaji maeneo karibu na vyanzo vyetu vya maji lakini vina muda. Muda ambao unapaswa kutumika ni muda ule wenye high season, maji yanakuwa mengi na muda huu wa kiangazi vile vibali huwa vina-expire. Sasa wale wamwagiliaji wamekuwa wakiendelea.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa hivi kama Wizara tayari tumeweka task force kuhakikisha hakuna atakayetumia maji yale kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji na shughuIi nyingine yoyote isipokuwa kuelekeza maji katika mitambo yetu kwa ajili ya kuchakata kwenda kwenye matumizi ya kibinadamu.
Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine wa Wizara yetu ni kuona tutaendelea kutoa elimu ya kutosha, matumizi sahihi ya maji katika maeneo yote yenye mito tiririka ili vyanzo vyetu vya maji visiweze kuathirika kama ulivyosema. Tayari tumeshatumia fedha nyingi kujenga miundombinu ambayo Serikali inatarajia wananchi waweze kupata maji ya kutosha, safi na salama wakati wote. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved