Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rehema Juma Migilla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Ulyankulu – Uyui hadi Tabora Manispaa kwa kiwango cha lami ikizingatiwa kuwa barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Wilaya hizo tatu?
Supplementary Question 1
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu hayo ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, suala la barabara hii limekuwa sasa kama ni hadithi. Hata watangulizi wangu wamekuwa wakipigia kelele sana barabara hii lakini pamoja na umuhimu wake bado Serikali inatuletea hadithi ya kwamba inatafuta bajeti. Wananchi wamechoka na hii hadithi, wanataka wajue je, ni lini barabara hii sasa itawekwa kwa kiwango cha lami?
Swali la pili; kwa kuwa Serikali bado inaendelea kutafuta bajeti kwa hii barabara lakini barabara hii ni muhimu sana, inapitisha mizigo kutoka sehemu mbalimbali na inapitisha abiria na mambo mengine. Lakini barabara hii mpaka leo inatumika kama uchochoro kwa baadhi ya magari ambayo yanakwepa kupima uzito sehemu nyingine. Sasa je, Serikali ipo tayari kutujengea mzani ili barabara hii iweze kuwa katika ubora wake ule ule?
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Migilla kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza siyo kweli kwamba hizi ni hadithi nimesema tu kwamba kwa niaba ya Serikali tunaendelea kutafuta fedha tufanye upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tuweze kujua tunahitaji upana wa lami kiasi gani na uzito wa mizigo unaoweza kupita katika eneo hilo, madaraja, ili tupate makisio ya bajeti ili tuweze kutafuta fedha. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira katika wakati huo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameomba mizani. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa wazo hili limepokelewa na litafanyiwa kazi na watapata majibu kwa wakati muafaka. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved