Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: - Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano wa Halotel katika Kata ya Chilangala ambapo mkataba ulisainiwa mwaka 2020 lakini mpaka Septemba, 2021 mradi huo haujaanza?
Supplementary Question 1
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza:
Mheshimiwa Spika, changamoto ya mawasiliano iliyopo Kata ya Chilangala inafanana na Kata za Kitaya, Mnongodi na Namtumbuka ambazo zipo mpakani na Msumbiji na ambako kama utakuwa unafahamu sasa hivi kuna changamoto ya kiusalama kule. Naomba mpango mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba Kata hizi kwa sasa zinakuwa na mawasiliano ya uhakika ili isaidie katika…
SPIKA: Zipo kwenye Wilaya gani hizi Kata.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, zipo Wilaya za Mtwara Vijijini na Tandahimba ambazo zinapakana na jirani zetu wa Msumbiji. Kwa hiyo naomba mpango wa haraka wa Serikali wa kuhakikisha kwamba Kata hizi zote zinapata mawasiliano ya uhakika.
Swali langu la pili ni kwamba minara ambayo inajengwa vijijini sasa hivi ni kwa ajili ya mawasiliano ya sauti tu, kwa ajili ya voice, lakini kuna mahitaji makubwa ya internet sasa hivi vijijini na hata Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inasema tunataka kuboresha upatikanaji wa internet vijijini. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuboresha au ku-upgrade minara hii ili iweze kuhakikisha kwamba hata data zinapatikana vijijini?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARl: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitumie fursa hii kuwapongeza sana Wabunge wote wa Mtwara kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia tunapofika katika maeneo yao ya kazi. Maeneo haya ya Kitaya pamoja na maeneo mengine ya Lulindi, Tandahimba pamoja na Newala tulishafika na kupitia fedha ambayo Serikali ilipitishiwa hapa Bungeni tayari kuna miradi ambayo imepangwa kwenda kutekelezwa kupitia miradi ya mipakani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi kabisa, kwa sababu dhamira ya Serikali ni ileile ya kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata mawasiliano. Maeneo ya mipakani tunayaangalia kwa umuhimu wake kwa sababu ni masuala ya kiusalama.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika Kata ya Kitaya, Mbunge anafahamu, mimi na yeye tulikwenda mpaka katika Kata ya Kitaya ambapo kuna mradi wetu ambao umeshakamilika na tayari umeshawashwa na huduma ya mawasiliano tayari imeshafika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala la uhitaji wa internet kwanza kabisa mpaka sasa Serikali inaboresha miundombinu ya Mkongo wa Taifa. Kwa upande wa Kusini mpaka sasa ukitoka pale Mangaka kwenda Mtambaswala takribani kilometa 72, tunajenga mkongo wa Taifa siku za hivi karibuni mradi huo utakamilika. Hivyo basi, hata ile miradi sasa ambayo itakuwa inahitaji data maana yake ni kwamba Serikali imeshaelekeza watoa huduma wote wahakikishe miradi yote ambayo itajengwa kuanzia sasa iwe inatoa huduma ya 3G na 4G na kuendelea. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved