Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Husna Juma Sekiboko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: - Wanawake na Watoto wanapata shida Baba wa familia anapofariki; pamoja na Sheria ya Mirathi; Je Serikali ina mpango gani zaidi wa kumsaidia mjane katika masuala ya mirathi?
Supplementary Question 1
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nishukuru kwa majibu hayo lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa msimamizi wa miradhi kwa mujibu wa sheria ya sasa anachaguliwa kwenye kikao cha familia ya marehemu ambacho katika kikao hicho mjane anakuwa ni mgeni, wengi wanakuwa ni ndugu wa marehemu, na hivyo anakosa kauli ya kuweza kuchagua au kupitisha mrithi au msimamizi wa mirathi hali inayopelekea familia kwa maana ya mjane na watoto kutaabika pale ambapo aliyechaguliwa kujimilikisha mali hizo. Je, ni lini sasa Serikali inatuletea marekebisho ya sheria hii ili tuweze kuondoa changamoto hizi?
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na sheria ambayo inakwenda kurekebishwa, je, Wizara inachukua hatua gani za dharula ili kuondoa hizi changamoto kwa sababu tunajua mchakato wa kurekebisha sheria inaweza kuchukua muda kidogo? (Makofi)
Name
Geophrey Mizengo Pinda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Answer
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Husna kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa inatokea wakati wa vikao vile vya familia za marehemu wajane hawa wamekuwa hawahusishwi kwa asilimia 100 katika kufika muafaka wa kupata yule Msimamizi wa Mirathi. Lakini kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba msimamizi wa mirathi, si mrithi wa mali za marehemu. Na kwa bahati mbaya sana, kwa kuwa sheria hii ya mirathi ina sura tatu yaani kuna sheria ambayo inaruhusu mfumo wa kidini katika kugawa mali, kuna kimila na kuna sheria ile ya Serikali; kumekuwa na mkanganyika mkubwa na ndiyo maana Serikali sasa kwa makusudi kabisa tumeamua kuzipitia hizi taratibu zinazosimamia mgao wa mirathi ili kuondoa huu mkanganyiko ambao kwa sasa unakabili familia nyingi sana.
Mheshimiwa Spika, lakini ni hatua gani za dharula ambazo tunazichukua, kwa sasa tunaendelea kila tunapopata nafasi ya kwenda katika maeneo mbalimbali ya nchi kuelekeza na kutoa elimu kwa wahusika wote. Kwamba ni muhimu wakatambua kuwa wasimamizi wa mirathi si warithi wa mali za marehemu, labda atokane na wale wanaotajwa kwenye orodha ya mirathi, na yeye anaingia kwenye ule mgao wa kawaida wa mali za marehemu. Lakini vinginevyo tumekuwa na tafsiri ambayo asili yake inatokana na mfumo wa kikabila na mila na desturi zao; yaani mtu akishaambiwa yeye ni msimamizi wa mirathi anajimilikisha haki zote za usimamizi wa mirathi na kuanza kutumia mali za marehemu.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwaomba na Waheshimiwa Wabunge po pote mtakapokwenda kuendelea kuelimisha, wakati sheria inakuja kuendelea kuelimisha juu ya nafasi ya msimamizi wa mirathi. Na inapobainika, kwamba, msimamizi wa mirathi ametumia kula mali ya marehemu kinyume cha utaratibu afikishwe kwenye vyombo vya sheria na hatua zichukue mkondo wake. Ahsante. (Makofi)
Name
Neema Kichiki Lugangira
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: - Wanawake na Watoto wanapata shida Baba wa familia anapofariki; pamoja na Sheria ya Mirathi; Je Serikali ina mpango gani zaidi wa kumsaidia mjane katika masuala ya mirathi?
Supplementary Question 2
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, kwa kuwa matatizo na changamoto ambazo wanapitia wanawake kwenye masuala haya ya kifamilia yamezidi kukithiri, na tarehe 6 Oktoba, 2021 Mheshimiwa Rais alilikazia hili, na hata Jaji Mkuu alielezea umuhimu wa kuwa na Mahakama ya Familia. Ningependa kuiuliza Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria. Je, ni lini ambapo itakuja na Mahakama ya Familia ili masuala yote haya ya mirathi matunzo na kadhalika yaweze kuangaliwa kwa utaratibu na haki iweze kutolewa? Ahsante.
Name
Geophrey Mizengo Pinda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Answer
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa mapendekezo mbalimbali yalitolewa kwa ajili ya kuanzisha Mahakama ya Familia, na bado tunaendelea kufanyia kazi, kwa sababu ni taasisi ambayo inahitaji kuwa kwenye muundo sasa wa utendaji kama zilivyo Mahakama nyingine. Kwa hiyo, ni imani yangu kwa kuwa tunakwenda sasa katika kurekebisha sheria yenyewe na muundo wake tunadhani tutakapokuwa tunakuja tutakuja na sura sasa ya kuwa na mahakama hii ambayo itashughulikia masuala ya mirathi. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved