Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. David Mathayo David
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Same Magharibi
Primary Question
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: - Barabara ya Mlimani kutoka Mwembe – Mbaga hadi Mamba - Myamba ni kero kubwa kwa wakazi zaidi ya 150,000 katika Majimbo ya manne; Same Magharibi na Same Mashariki ambapo zaidi ya 70% ya wakazi wake wanaishi milimani. Je, ni lini barabara hiyo yenye urefu wa Km 120 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami nyepesi (Surface dressing) ili kufanikisha shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Same?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru majibu ya Mheshimiwa Waziri kidogo yanaleta matumaini kwa mbali, lakini kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne japo haijawahi kuwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi; lakini kwa kuwa TANROADS kila mwaka inapoteza mabilioni ya fedha, kwa mfano mwaka huu barabara hii imetengewa shilingi bilioni mbili, lakini vifusi vipowekwa baada ya mvua kunyesha usiku mmoja tu, kifusi hiki kinazolewa na maji ya mvua na wananchi wa milimani ambapo ni asilimia zaidi ya 65 ya wakaazi wa Wilaya ya Same wanakosa mawasiliano na pia Serikali inaingia hasara: -
Je, upembuzi yakinifu wa barabara hii utafanyika lini ili Serikali isipoteze mapato lakini wananchi wa Mwembe, Mbaga, Bonja mpaka Mamba waweze kupata mawasiliano pale mvua zinaponyesha? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Tunafahamu kwamba Sera ya Serikali ni kuunganisha mikoa kwa mikoa na Wilaya kwa Wilaya; vile vile nchi hii na Wilaya hizi za nchi hii kuna tofauti ya mazingira, kwa mfano Wilaya ya Same kuna malima mingi sana, Lushoto kuna milima mingi; Mbinga kuna milima; Kagera na maeneo ya Arusha kuna milima mingi sana: Sasa kwa nini Serikali isichukue ikafanya upembuzi yakinifu wa barabara zote za milimani kusudi wananchi wa milimani waweze kupata usafiri wakati mvua zinanyesha? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwenye maeneo ya miinuko vifusi huwa vinasombwa na maji. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna barabara za lami na za changarawe na za udongo. Azma ya Serikali ni kuwa na barabara zote za lami, lakini uwezo huo bado hatujakuwa nao na kwa hiyo Serikali inatengeneza barabara kwa kiwango cha lami, kila mwaka tunatenga fedha ili barabara hizo ziweze kutumika.
Mheshimiwa Spika, bajeti aliyoisema ya bilioni mbili siyo tu kuweka kifusi, ni pamoja na kutengeneza mifereji, madaraja pamoja na makalavati ili barabara hiyo iweze kutumika kwa mwaka mzima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema, tunatafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na hatimae usanifu wa kina.
Mheshimiwa Spika, pengine nitoe maagizo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro aweze kuainisha yale maeneo yote korofi na yenye miinuko mikali ili tuweze kufanyia matengenezo surface dressing ama hata kujenga barabara hizo kwa zege kama ilivyofanyika maeneo mengine kama Mikoa ya Manyara, Ruvuma, Kigoma, ukienda Morogoro; maeneo ambayo ni korofi basi barabara zinajengwa kwa kiwango hicho.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu mikoa, ni kwamba kama tulivyoainisha kwamba tunaunganisha mikoa na mikoa kwa kiwango cha lami, hiyo ndiyo sera ambayo tunayo, lakini wazo la maeneo kwenye miinuko, basi tulichukue na tukiona kama fedha itatosha, basi Serikali itafanya hivyo. Azma ni kuhakikisha kwamba barabara zote zinajengwa kwa kiwango cha lami bila ya kujali eneo eneo na eneo. Ahsante. (Makofi)
Name
Anne Kilango Malecela
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Primary Question
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: - Barabara ya Mlimani kutoka Mwembe – Mbaga hadi Mamba - Myamba ni kero kubwa kwa wakazi zaidi ya 150,000 katika Majimbo ya manne; Same Magharibi na Same Mashariki ambapo zaidi ya 70% ya wakazi wake wanaishi milimani. Je, ni lini barabara hiyo yenye urefu wa Km 120 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami nyepesi (Surface dressing) ili kufanikisha shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Same?
Supplementary Question 2
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika nashukuru kwa kupata nafasi. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kutumia pesa nyingi sana kujenga Daraja la Yangoma ambalo lilikuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi waliopo kwenye barabara hii. (Makofi)
Mheshimwia Spika, kulingana na ubora wa Daraja la Yongoma lililojengwa ambalo Naibu Waziri, Mheshimiwa Waitara, alikuja tukaenda kuliona. Kweli Serikali hamwoni kuna umuhimu wa kuijenga ile barabara iwe na hadhi sawa na lile daraja lililowekwa pale? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru kwa kupongeza kazi nzuri ambayo imefanyika ya kujenga lile daraja. Pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kujenga daraja hilo maana yake ni maandalizi ya kuja kujenga pia barabara nzuri inayofanana na hilo kwa sababu hatutajenga tena.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kwenye jibu letu la msingi tumesema tunatafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili sasa hiyo barabara iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Hiyo hatua hatuwezi kuiruka, ni lazima tuifanye na ndiyo maana tunatafuta hiyo fedha. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved