Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Michael Mkundi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la mawasiliano ya simu katika maeneo ya Bukiko, Chabilungo, Kitale na maeneo mengine yenye tatizo hilo Visiwani Ukerewe?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwanza kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini eneo la Bukiko ni kweli kupitia UCSAF, ulijengwa mnara wa Halotel lakini kuna shida kubwa; ule mnara unategemea umeme jua, kiasi kwamba nguvu ya umeme inapopungua kunakuwa hakuna mawasiliano, lakini vile vile kuna shida kubwa ya Internet kwa sababu mtandao ulioko pale ni wa 2G; Sasa naiomba Serikali niweze kujua, ni lini sasa Serikali itapeleka jenereta kwenye eneo lile? Vile vile iwasiliane na watu Halotel ili kuweka mtandao wa zaidi ya 2G kwa maana ya 3G na vyovyote itakavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kwenye majibu, ni kweli kuna shida kubwa ya mawasiliano kwenye maeneo mengi, kwenye visiwa vya Ukerewe; na Serikali imejibu kwamba itaenda kupitia maeneo yote yenye shida: Ni lini sasa kazi hii itafanywa na Serikali ili timu iende kule, ifanye uchunguzi na hatimaye marekebisho yafanyike ili kuwe na mawasiliano mazuri kwenye eneo lile? Nashukuru sana. (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu jenereta; kwanza kabisa ile site ya mawasiliano iwe imekamilika, haijalishi kama ni umeme wa TANESCO au ni wa Solar, ni lazima site iwe na backup generator. Kwa vile Mheshimiwa Mbunge amelifikisha hili, basi Serikali inalipokea na tutalifanyia kazi ili kujiridhisha na changamoto ambayo ameiongea.
Mheshimiwa Spika, vilevile ni azma ya Serikali sasa kuhakikisha kwamba, maeneo mengi nchini yanapata huduma ya internet, yaani kutoka katika huduma ya zamani ya 2G kwenda 3G. Hapo kabla Wizara tayari ilishatoa maelekezo kwa watoa huduma ili kuhakikisha kwamba, minara inayojengwa kuanzia sasa basi iwe na huduma ya 3G.
Mheshimiwa Spika, tuna minara ya aina mbili; minara ambayo inatokana na ruzuku ya Serikali, lakini vilevile kuna minara ambayo inatokana na wawekezaji wenyewe. Ile ambayo inatokana na ruzuku ya Serikali tayari Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeshaanzisha mchakato wa ku-up grade minara yote ambayo itakuwa ina 2G kwenda kwenye 3G. Pia Serikali imeelekeza kwa watoa huduma wengine katika minara ambayo sio ya Serikali, ihakikishe kwamba, inaona umuhimu sasa wa kuelewa kwamba, sasa teknolojia ya 3G inahitajika kwa Watanzania wote. Ahsante.
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la mawasiliano ya simu katika maeneo ya Bukiko, Chabilungo, Kitale na maeneo mengine yenye tatizo hilo Visiwani Ukerewe?
Supplementary Question 2
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Hivi karibuni na katika Jimbo lote la Ndanda kuna matatizo sana ya network na hasa eneo la Ndanda ambako ndio Makao Makuu ya Jimbo na mtandao tunaotumia pale sana ni Vodacom pamoja na Airtel na Airtel kuna hisa za Serikali. Hata hivyo, wataalam walipopewa taarifa mpaka leo hawajaenda kufanya marekebisho. Sasa kwa nini Mheshimiwa Waziri asiwakumbushe watu wa Airtel kwenda kuufanyia marekebisho mnara ule ili mawasiliano yawe bora?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kimsingi ameomba Serikali tuongee na watu wa Airtel ili wakarekebishe changamoto iliyojitokeza. Tunaipokea changamoto hiyo na tutawasiliana na wenzetu wa Airtel ili kwenda kuifanyia kazi hiyo changamoto. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved