Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Eng. Ezra John Chiwelesa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Primary Question
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Burigi – Chato ili waache kuingiza Mifugo ndani ya Hifadhi na kumaliza mgogoro kati ya wananchi hao na Hifadhi hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa na tatizo kubwa sana katika eneo hili la hifadhi hii ya Burigi Chato na tunashukuru kwa fedha ambazo zimetolewa na kutoa elimu kwa umma unaozunguka hifadhi ile. Kumekuwa na kesi kubwa sana pale za mifugo ya watu kukamatwa ndani ya hifadhi lakini baada ya kukamatwa zinapopelekwa kesi mahakamani, watu wale wamekuwa wanatozwa fine ya Shilingi 100,000/= kwa kila ng’ombe na wengi wanalipa baada ya kutozwa ile fine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa shida imekuja unatoza fine mahakamani ulikamatiwa ng’ombe 100 unapopewa barua ya mahakama, umeshalipa fedha ya Shilingi Milioni 10 ukarudishiwe ng’ombe wako unaenda unakuta ng’ombe wako 70, ng’ombe wako 80 badala ya ng’ombe waliokamatwa.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba kusikia kauli ya Serikali juu ya vitendo hivi ambavyo vimesababisha wananchi wa Biharamulo kuteseka na hatimae kupoteza fedha zao na ng’ombe hao ambao wamekuwa wanapotea huko. Nisikie kauli ya Serikali juu ya hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kumekuwa na kesi pia wananchi wananifuata ninapokuwa Jimboni, saa nyingine wanapiga simu na kwa DC kesi zipo. Mwananchi anakuja analalamika kwamba, Mheshimiwa Mbunge nimekamatiwa ng’ombe wangu 50 bado tuna kesi mahakamani, lakini ng’ombe wangu nimewaona kwenye mnada wanauzwa. Sasa naomba kusikia kauli ya Serikali juu ya hili jambo ambalo limesababisha watu sasa wanaona taabu kabisa na wanatuchonganisha na wananchi. Tukisikia kauli ya Serikali juu ya hili pia hao ng’ombe ambao wamekuwa wanauzwa kwenye mnada je, hatuoni haja ya Serikali kuunda Tume Maalum, kwa ajili ya kwenda kuangalia hivi vitendo vya wananchi kulalamika? Kwamba, ng’ombe wao wanauzwa kwenye mnada na ilhali bado kesi zinaendelea mahakamani.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika,
ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza niendelee kutoa pole kwa wale wananchi ambao wameendelea kukutana na kadhia hii, ya kudhulumiwa mifugo yao na kumekuwa ndiyo na malalamiko mengi na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walishawahi kunifuata kwamba, kuna baadhi ya wahifadhi wasio waaminifu ambao inapelekea mifugo yao kutotimia kama ambavyo imekamatwa awali.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tunafahamu Sheria za Utumishi wa Umma, watumishi hawa tumekuwa tukiwachukulia hatua wale ambao wanahusika na kadhia hii ikiwemo upotevu wa mifugo. Lakini pia kumekuwa na changamoto ya baadhi ya mifugo ambayo huwa inakufa wakati ikiwa inasubiri kupelekwa Mahakamani kwa maana ya kesi inapochukua muda mrefu Mahakamani inapelekea baadhi ya mifugo kupoteza maisha. Lakini kwa upande mwingine ambao amesema Mheshimiwa Mbunge kwamba mifugo mingine inaonekana iko minadani, basi Serikali itaendelea kufuatilia na wale watumishi ambao wanahusika na changamoto hizi tutawachukulia hatua. Na inapothibitika basi wengine tunawasimamisha kazi na hata kufukuzwa kazi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge ambao wana changamoto hii, niwaombe pale kuna mfugaji ambaye amekutana na changamoto hii basi watusaidie kutupa hizi taarifa. Lakini pia niwaombe Waheshimiwa tuendelee kuelimisha hawa wafugaji pia, wakifuga kwa kufuata Sheria na taratibu za nchi ninaamini kabisa kadhia hii tutaipunguza kabisa ama kuimaliza. Ahsante. (Makofi)
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Burigi – Chato ili waache kuingiza Mifugo ndani ya Hifadhi na kumaliza mgogoro kati ya wananchi hao na Hifadhi hiyo?
Supplementary Question 2
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, katika harakati za Serikali kuhifadhi mazingira na maliasili yetu ilihamasisha wananchi kufungua mabucha ya wanyamapori. Wananchi wa Jimbo langu walihamasika na walifungua mabucha tatizo ni upatikanaji wa leseni kutoka Wizara husika.
Je, ni lini wananchi wangu watapatiwa leseni ili shughuli hii ya kuuza nyamapori iweze kuanza ndani ya Wilaya yangu?
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imeendelea kutoa leseni za mabucha kwenye maeneo mbalimbali ya hapa nchini na hizi bucha ni kwa ajili ya wanyamapori. Mwaka wa fedha 2020/2021 tuliweza kutoa leseni zaidi ya 46 na tuna masharti ya namna ambavyo wanapaswa kuomba hawa wafanyabiashara wanaofanya biashara hizi za wanyamapori. Lakini kumekuwa na changamoto ya ukosefu wa wanyamapori wenyewe, kwa maana unapowinda kuna- target ambazo wanazifahamu wawindaji. Sasa kumekuwa na malalamiko kwa wale wenye leseni wanakosa nyama na matokeo yake wanarudisha wanashindwa kuendelea na biashara hii.
Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kama kuna yeyote ambaye anahitaji leseni, Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari wakati wowote kutoa leseni. Lakini changamoto inayojitokeza ni kwamba upatikanaji wa wale wanyama wenyewe ndiyo changamoto halisi inayojitokeza. Kwa sababu, uwindaji kuna maeneo ambayo tunayatenga lakini inapokosekana basi malalamiko yanarudi kwa Serikali, lakini leseni zipo tunawakaribisha wafanyabiashara wote waje. (Makofi)
Name
Ndaisaba George Ruhoro
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Primary Question
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Burigi – Chato ili waache kuingiza Mifugo ndani ya Hifadhi na kumaliza mgogoro kati ya wananchi hao na Hifadhi hiyo?
Supplementary Question 3
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Kwa kuwa, ukosefu wa vitalu vya kufugia mifugo na maeneo ya malisho ndio sababu kubwa ya kupeleka mifugo hifadhini na kwa kuwa, elimu inayotolewa na Wizara ya Maliasili inatolewa kwa binadamu na siyo ng’ombe na kwa vile ng’ombe wao wanataka kula majani na wakati wa kiangazi hakuna sehemu ya majani na majani yako porini.
Je, Wizara ina utaratibu gani ama ina mpango gani wa kuhakikisha eneo lile la hifadhi linamegwa, tunapata vitalu kwa ajili ya kufugia mifugo yetu ng’ombe kwa upande wa Biharamulo na Ngara? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya ukosefu wa malisho na imepelekea kuwepo na migogoro baina ya Wahifadhi na Wafugaji. Serikali inatambua changamoto za ukosefu wa maeneo ya mifugo, lakini kupitia Kamati ya Mawaziri Nane ambao tumekuwa tukizunguka nchi nzima, tayari Serikali imetoa maeneo ambayo yatamegwa kwa ajili ya wananchi kutumia. Hivyo tunaendelea kuelekeza wananchi wayatumie vizuri ikiwemo kutenga maeneo hayo kwa ajili ya malisho na kuandaa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya wafugaji na matumizi kwa ajili ya kilimo. Hivyo, Serikali imeshaliona hili na tumeendelea kutoa elimu lakini pia kumega maeneo ya hifadhi. (Makofi)