Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Kasheku Musukuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Primary Question
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa kilometa 20 kutoka Nkome hadi Nzera?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Barabara inayotoka Geita kwenda Nkome ina kilometa 57 na ilishafanyiwa upembuzi yakinifu muda mrefu na ikawekwa mpaka beacon na alama za kuanza mkandarasi. Leo tunazungumza ni karibia mwaka wa pili, tunaahidiwa kila siku: Ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kuuona Mji wa Nzera ambao ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri ya Mji wa Geita; haijawahi kuona lami; kila mwaka tunaahidiwa na leo ni mwaka wa nne?
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Barabara ya Kamanga – Sengerema – Buchosa – Nkome ni barabara ambayo imeng’oa Wabunge zaidi ya sita, upande wa Sengerema na upande wa Buchosa; lakini tumekuwa tukipata ahadi zilezile za Serikali kwamba mwakani tunajenga, mwakani tunajenga; sasa nataka kumwuliza Mheshimiwa Waziri, tufundishe njia ambayo unaona ni nzuri na sisi tupite kama ni dirishani angalu tupate hiyo lami. Bado tunapenda kuendelea kuwa Wabunge.
Naomba commitment ya Serikali, ni lini mtaanza kutengeneza Barabara ya Kamanga – Sengerema – Buchosa – Nkome?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, beacon zilizowekwa haikuwa usanifu wa kina; na fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka huu tunaoutekeleza inakwenda kufanya kazi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, yako maandalizi ambayo yanaendelea kwa ajili ya kuanza huo mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina yakiwa ni maandalizi ya kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, barabara hii ya pili aliyoisema ya Kamanga – Sengerema – Buchosa hadi Nkome, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba itatekelezwa kama ilivyoahidiwa kwenye Mpango wetu na kama ilivyoelezwa kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka 2020 - 2025. Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kutafuta fedha na ikipatikana hizi barabara zote zitajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved