Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Primary Question

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mhe. Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2018 ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilombero?

Supplementary Question 1

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya kutelekeza ahadi hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu maana Waziri Mkuu mwenyewe alilitembelea eneo hili na aliona ufinyu wa eneo hili. Napenda pia kuishukuru Serikali kwa Waziri wa Ardhi Mheshimiwa Lukuvi kutupatia ardhi Kata ya Kiberege kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hii ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa sasa hivi wakati mchakato wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ukiendelea Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara wanategemea sana kituo cha afya cha Kibaoni, kituo hiki kinakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi.

Je, Serikali haioni kuchukua hatua za haraka kuongeza watumishi katika kituo cha afya cha Kibaoni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kutokana na ufinyu wa ardhi na eneo la ekari takribani kumi za kujenga Kituo cha Afya cha Kata ya Ifakara Mjini, Ifakara Mjini mpaka sasa hivi haina Kituo cha Afya eneo lililopo ni dogo. Je, Serikali ipo tayari kutupatia ramani maalumu ya ujenzi wa ghorofa ili tufanye mchakato wa kuanza Kituo cha Afya cha Kata ya Ifakara Mjini?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee shukrani zake nyingi kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi ambayo imeendelea kuifanya ya kujenga vituo vya afya, hospitali na zahanati nchini kote na nimuhakikishie kwamba mpango huo ni endelevu tutaendelea kujenga vituo vya afya, zahanati, lakini na hospitali zetu za halmashauri kuhakikisha tunasogeza huduma za afya kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kituo cha afya cha Kibaoni kuwa na watumishi wachache nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi wa vituo hivi unakwenda sambamba na mipango ya kuajiri watumishi kwa awamu kwa kadri fedha zitakapopatikana, lakini pia kwa kadri ya vibali vya ajira vitakavyotolewa. Kwa hiyo, naomba nichukue suala hilo na tutakipa kipaumbele kituo cha afya cha Kibaoni ili kiweze kupata wahudumu kwenye awamu za ajira zinazofuata ili tutoe huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kituo cha afya Ifakara Mjini utaratibu upo wazi kama tunahitaji kujenga jengo la kwenda juu kwa maana ya ghorofa. Tunaomba kibali rasmi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunawasilisha michoro na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia watalaamu tunapitia na kuwashauri namna ya kujenga. Kwa hiyo tunakukaribisha kuwasilisha maombi hayo ili tuweze kuona uwezekano wa kujenga kituo hicho. Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mhe. Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2018 ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilombero?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kituo cha Afya cha Mwaya – Mahenge – Ulanga majengo yake yamejengwa kwa muda mrefu na ni mabovu. Je, ni lini kitafanyiwa ukaratibu Kituo cha Afya hiki cha Mwaya? Ahsante sana.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa DKt. Christine Ishengoma Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vituo vyetu na hospitali zote za halmashauri chakavu ambazo zimejengwa muda mrefu zinaandaliwa utaratibu wa kwenda kuzifanyia ukarabati. Kwa hivyo tumeshaanza na utaratibu wa hospitali za halmashauri, tumeshazitambua hospitali 23 kongwe, lakini tutakwenda kutambua vituo afya chakavu vya siku nyingi ili tutafute fedha kwa awamu kwa ajili ya kuvifanyia ukarabati, lakini pia kuvifanyia upanuzi wa vituo vile. Kwa hiyo, naomba nimuhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati zoezi hilo linafanyika tutahakikisha pia Kituo cha Afya cha Maya kinapitiwa na kufanyiwa tathimini hiyo. Ahsante.