Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:- Ukatili kwa watoto umekithiri nchini kama vile ubakaji, ulawiti, kuchomwa moto na mimba za utotoni. (a) Je ni watoto wangapi wamefanyiwa ukatili huo kwa jinsia zao wa kike na wa kiume? (b) Je kuna takwimu halisi ya hatua zilizo chukuliwa na Serikali dhidi ya matukio hayo nchini?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza kwanza kwa takwimu tu za Serikali inaonyesha ni kwa jinsi gani ukatili dhidi ya watoto ni mkubwa sana kwenye nchi yetu ya Tanzania ambayo inaenda kinyume na mkataba wa kimataifa ambao tumeingia wa haki za watoto.
Mheshimiwa Spika, takwimu ambayo Serikali imetoa ni za kuanzia januari tu mpaka Septemba, 2021. Sasa asikwambie mtu kama angetoa uanzia za miaka mitatu au minne nyuma inamaana ni janga kubwa sana na hii inaonyesha dhahiri kwamba kuna changamoto ya uratibu ya takwimu maana hapo umetoa sources moja tu kutoka polisi wakati najua kuna sehemu kama Kamati MTAKUWWA, ukienda kwenye ustawi wa jamii, ukienda kwenye mashirika ya siyo ya Kiserikali lakini hata zile familia ambazo zinamalizana juu kwa juu ukikusanya haya matukio mengi takwimu ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ninataka kujua ni utaratibu gani Serikali imeuweka ya kuhakikisha kwamba inatoa takwimu halisia na kwa wakati kutoka kwenye vyanzo vyote hivi ili kuweza kuwasaidia watoto wa Kitanzani kujua ukubwa wa tatizo ni nini kuliko ku-base kwenye polisi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na kusua kusua kutokutenga au tukitenga kupeleka fedha kwenye utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilataka kujua ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanatenga bajeti ya kutosha na wanaitekeleza kuhakikisha kwamba kuna kuwa na madawati ya kijinsia ya kutosha kuanzia ngazi ya mitaa, wanawawezesha kuwa na Maafisa Ustawi wa Jamii, Kamati ya MTAKUWWA inapata fedha za kutosha ili kutokomeza hii tatizo kubwa la unyanyasaji wa watoto wa Kitanzania ambao wanabakwa, wanalawitiwa, wanauwawa, wanachomwa moto, ahsante sana. (Makofi)
Name
Jenista Joackim Mhagama
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Peramiho
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
nimpongeze kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri na ninadhani liko suala linalohusu takwimu za unyanyasaji ataendelea kuzijibia.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ninaomba tu nitoe maelezo mafupi kuhusu mkakati huu wa kitaifa wa mapambano dhidi ya unyanyasaji kwa wanawake na watoto kwa sababu Ofisi ya Waziri Mkuu imepewa jukumu la kuratibu na kuziunganisha sekta na utekelezaji wake ukifanywa na Wizara yenye dhamana ya Afya Maendeleo ya Jamii, Wazee, Wanawake na Watoto.
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na mkakati wa kwanza ambao ulizinduliwa mwaka 2016 mkakati huo wa MTAKUWA na lengo kubwa ilikuwa ni kukidhi matakwa ya kimataifa lakini matakwa ya Taifa vile vile kuhakikisha kwamba tunaweka sawa masuala haya ya unyanyasaji wa wanawake na Watoto na mkakati huo wa kwanza ndiyo unafikia mwisho, unaelekea kufikia mwisho mwaka 2021/2022 tutakuwa tumeumaliza.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni hivi majuzi tu, wiki mbili zilizopita, nilikuwa kwenye kikao cha wataalam kufanya tathmini ni kwa kiasi gani MTAKUWWA I imeweza kufanikiwa. Masuala yaliyoelezwa na Mheshimiwa Mbunge tumeyaona kwamba ni masuala ambayo yameleta utatanishi kidogo kwa namna moja ama nyingine katika utekelezaji wa MTAKUWWA.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namhakikishia kwamba kwenye mkakati wa pili sasa masuala ya bajeti, masuala ya madawati na ya rasilimali watu katika kuhakikisha MTAKUWWA II inafanikiwa na inafikia malengo ambayo yalikusudiwa yanazingatiwa sasa katika mkakati huu uliopita ambao unafanyiwa tathmini, lakini mkakati utakaokuja haya yote yatazingatiwa.
Mheshimiwa Spika, naomba niwape pongezi sana wenzetu wa Jeshi la Polisi. Wameanzisha madawati mengi ya kutosha katika maeneo mbalimbali kwenye vituo vyao vya polisi kwa ajili ya kusaidia kuhakikisha wanawake na watoto wanapata haki zao. Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa MTAKUWWA kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutakuja muda ukifika tutaomba ushauri, maoni na hata kwa Waheshimiwa Wabunge ili MTAKUWWA II uweze kufanikiwa kwa kadri ya mpango tuliokusudia kuwaokoa wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji katika nchi yetu. Nakushukuru. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved