Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: - Utoaji wa leseni za biashara kwa biashara ndogo za maduka katika Manispaa ya Kinondoni umekuwa na changamoto kutokana na wafanyabiashara hao kutokuwa na Tax Clearence kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Je, ni kwa nini Serikali isiiagize TRA kwenda mitaani na kubaini biashara hizo na kuzisajili kwa lengo la kurahisisha utoaji wa Tax Clearance ili leseni ziweze kutolewa?
Supplementary Question 1
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jitihada za kunijibu ingawa swali langu la msingi niliuliza ni lini sasa Serikali itakwenda mitaani, itashuka chini kwa maana ya TRA kuweza kuwabaini wafanyabiashara hawa waweze kuandikishwa na hatimaye waweze kupata tax clearance?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu tunaona kwamba, Serikali inasema kuna kampeni ya mlango kwa mlango, nataka nikiri, sijaiona kampeni hiyo na kwa hali hiyo kama utaratibu huo upo maana yake ni kwamba, utachelewesha sana kuweza kulifanya zoezi hili: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu; kwa kuwa, Serikali imeweza kufanikisha kuwepo kwa Maafisa kwenye kila kata, kwa mfano Maafisa wa Elimu, Maafisa Afya, Maafisa Kilimo, na kadhalika; ni kwa nini sasa Serikali isifikirie kuwa na Maafisa Kodi kwenye kila kata ili waweze kufanya kazi ambayo ni ya kuwafikia kwa urahisi wafanyabiashara ambao kila siku wanalalamikia masuala ya tax clearance na license? Kule Kinondoni shida ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; ili kuweza kuwabaini wafanyabiashara hasa hawa wadogowadogo katika maeneo yetu, je, Serikali haioni busara kama inaweza ikaanzisha madaftari katika kila mtaa kuweza kuwabaini wafanyabiashara ndogondogo ili matatizo yao ya elimu ya ulipaji wa kodi na masuala mengine yakatatuliwa kwa urahisi, badala ya kuzungumzia elimu ambayo inatolewa na mamlaka kupitia kwenye ofisi za kodi kiasi kwamba, si rahisi jambo hilo kuweza kutekelezeka zaidi ya nadharia? Ahsante sana.
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Abbas, Mbunge wa Kinondoni, kwa namna anavyowapigania na kuleta maendeleo katika Jimbo lake la Kinondoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Abbas, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza suala la kushuka chini ni kama ambavyo tumezungumza katika swali la mwanzo la Mheshimiwa Agnesta. Serikali yetu iko tayari kushuka chini kwenda hadi Serikali za Mitaa kwa ajili ya ukusanyaji wa kodi, lakini la kuanzisha maafisa ndani ya Serikali za Mitaa, hili tutachukua kama ni wazo na ushauri na tutautekeleza baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Abbas kwamba, kampeni ya mlango kwa mlango ipo na pengine tu kutokana na majuku yake mengi hajashuhudia. Hii ni kwa sababu, tayari mpaka kufikia tarehe 31 mwezi jana, basi walipakodi 432,323 ndani ya Kinondoni peke yake tumewasajili tayari na wafanyabiashara kati ya hao ni 171,973 kwa hiyo, suala hili la mlango kwa mlango liko Mheshimiwa Abbas. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved