Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Primary Question

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA Aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Madaktari Bingwa na vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete Mkoani Tabora?

Supplementary Question 1

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Kitete, kama neno rufaa linavyoonesha, ndio hospitali tegemezi kwa Mkoa wa Tabora. Hospitali ile inahitaji Madaktari Bingwa wasiopungua nane na kama alivyojibu Mheshimiwa Waziri kwamba, kuna Madaktari watatu, ingawa mimi nafahamu kuna Madaktari Bingwa wawili yani kama ilivyo jibu lake la msingi, kwa watoto na akinamama; hatuna Madaktari wa upasuaji, hatuna Madaktari wa mifupa, hata physician hawapo kwa hiyo, hatuna Madaktari wengi na hii ni hospitali ya rufaa. Niseme namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kutupa shilingi hizo bilioni 10.5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya dharura pamoja na majengo ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, baada ya Mheshimiwa Rais kutoa fedha zote hizo na majengo tayari yamekamilika, hayana Madaktari Bingwa kwa muda mrefu, Wizara ya Afya hamuoni mnaanza kudidimiza hata juhudi za Mheshimiwa Rais kwa kutoleta madaktari bingwa katika majengo hayo mazuri ambayo yanajengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, sehemu zingine kuna Madaktari Bingwa wengi sana, ikiwemo Dar-es-Salaam. Na kwa kuwa, Madaktari wengi hawaendi kwenye mikoa mingine kama Tabora kwa sababu ya vivutio. Je, Wizara imejipangaje kuweka vivutio kwa madaktari hawa bingwa ili waweze kuvutiwa kufanya kazi sehemu kama Tabora Mjini? ahsante.

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja amesema Madaktari ni wawili sio watatu; mimi ninachoweza kumwambia mpaka mwisho wa mwaka huu maana yake wanaenda kuongezeka Madaktari sita. Wanapoongezeka maana yake watakuwa, tulitegemea wawe tisa, lakini maana yake unasema watakuwa nane, lakini nataka kukuhakikishia watakuwa tisa mpaka tunapofika mwisho wa mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, specifically ametaja baadhi ya magonjwa na matatizo yanayowasumbua zaidi kwenye eneo lao; tayari Waziri wa Afya ameshaelekeza upembuzi yakinifu ufanyike nchi nzima kujua maeneo yenye Madaktari wengi kuliko mahitaji halisi, ili kuweza kuwapeleka katika yale maeneo ya pembezoni ambayo yana uhitaji zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amezungumzia suala zima la kwamba, la watumishi kwa ujumla kwamba, majengo yanakwenda kwisha na wakati mwingine majengo yanakuwa mazuri, lakini ndani yake hakuna watumishi wa kufanya kazi hiyo; lakini nimwombe Mheshimiwa Mbunge suala la watumishi wa afya kuwa wachache sio suala tu la Tabora peke yake ni suala la nchi nzima na ni tatizo ambalo hata wanapokwenda shuleni kuwa recruited wanakuwa vilevile wachache, kwa hiyo kwenye soko kuwapata aina ya kada unayotaka wakati mwingine ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwamba tumechukua; na hata wakati fedha hizi shilingi trillion 1.3 ambazo Mheshimiwa Rais wetu ameipa Sekta ya Afya shilingi bilioni 495, alielekeza kwamba wakati ujenzi huu unaendelea, vile vile tukae na TAMISEMI na kwa wakati huo huo tukae na Wizara ya Utumishi kujipanga kuhakikisha majengo yanapoisha na ujenzi huo unapoisha, watumishi wanapatikana wa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mwakasaka usiogope jinsi fedha na ikama inavyotoka. Tutahakikisha kila mahali kunakuwepo na watumishi wanaoweza kutoa huduma. Pia tunapunguza hilo tatizo kwa kuhakikisha vilevile madaktari bingwa walioko Dar es Salaam na mikoani wanaweza wakachukua wale wagonjwa wanaotakiwa kupelekwa rufaa Dar es Salaam au kwingine au kuletwa Benjamin, wakawafuata huko huko Kitete na kutibiwa huko huko ili kupunguza wananchi kuja Benjamin au kwenda Dar es Salaam. Ahsante sana.

Name

Humphrey Herson Polepole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Primary Question

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA Aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Madaktari Bingwa na vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete Mkoani Tabora?

Supplementary Question 2

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani; na ni lini itaanza kuwezesha majaribio ya kitabibu au kwa Kiingereza wanaita clinical trials kwa bidhaa za mimea dawa ambazo zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na mbadala na tayari
zinatumika kwa uhiyari wa wagonjwa kama over the counter drugs na zimeonyesha ufanisi mkubwa katika kutibu magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mfumo wa upumuaji? Ahsante.

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri. Labda nimwambie tu siyo kwamba ni lini itaenda kuanza, imekuwa ikifanya hivyo; na taasisi yetu ya NIMR na kushirikiana na wadau mbalimbali wamekuwa wakifanya hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnakumbuka kwenye fedha hizi ambazo zimetoka, shilingi trilioni 1.3, katika fedha hizo, shilingi bilioni 6.1 zilitengwa kwa ajili ya eneo hilo la tafiti ikiwepo na suala la tiba asili. Kama mnakumbuka hapa Bungeni, niliwahi kusema kwamba kuna kipindi Mheshimiwa Rais wetu alipeleka shilingi bilioni 1.2 pale NIMR kwa ajili ya kufanya mambo kama hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaulizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Rais wetu ameielekeza Wizara kwamba tuwekeze nguvu nyingi sana kwenye eneo hili la kufanya tafiti za madawa yetu ya asili kwa sababu yametusaidia sana kipindi kile ambapo tunapitia wakati mgumu kwenye Corona wakati hakuna anayejua suluhu ni nini kwenye tatizo hili. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA Aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Madaktari Bingwa na vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete Mkoani Tabora?

Supplementary Question 3

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi 1,500,000,000 tukajenga Hospitali ya Halmashauri. Sasa hospitali hii inafanya clinic ya watoto pake yake, haina vifaa tiba na hasa madaktari bingwa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta vifaa tiba ili hospitali ile ifanye kazi kama ilivyokusudiwa na Serikali?

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake mzuri wa masuala ya wilaya yake. Labda nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala siyo fedha za kununua bidhaa hizo, tayari Rais wetu ametoa fedha na sasa ni mchakato wa manunuzi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, nikimaliza muda wa maswali njoo tukae pamoja ili ueleze specifically na tuwasiliane na DMO wako ili aweze kutuletea list specifically kinachotakiwa ili kiweze kwenda kununuliwa na kufanyika haraka ili upate huduma hiyo. Ahsante sana. (Makofi)