Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Vita Rashid Kawawa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Primary Question
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwarudishia wamiliki halali silaha zao ambazo zilichukuliwa na Serikali wakati wa zoezi la Operesheni Tokomeza?
Supplementary Question 1
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; kwa kuwa kulikuwa na wananchi ambao walipata silaha hizo kihalali na kwa kufuata taratibu zote na walikuwa wanazilipia kila mwaka na wenyewe walitii amri kwa kuzipeleka katika vituo vya polisi na sasa Serikali imeamua hivyo isiwarudishie. (Makofi)
Je, Serikali inaweza sasa kuwarudishia thamani ya gharama ya silaha zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Jimbo la Namtumbo ni la wakulima na mashamba yao yamezungukwa na mapori yenye wanyama wakali na waharibifu na kwa kuwa Serikali awali dhamira yake iliwaruhusu kuwa na silaha hizo ili waweze kujilinda wao wenyewe na mali zao ambayo ni mashamba yao.
Je, Serikali sasa ina mpango gani mbadala wa kuweza kuwasaidia wakulima na wananchi hawa, kuepukana na adha wanayoipata ya kuharibiwa mazao yao na kuuawa na wanyama waharibifu na wakali? (Makofi)
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Kawawa, lakini pia niwapongeze sana wananchi wa Jimbo la Namtumbo kwa kuendelea kuwa na subira kwa jambo hili. Wamesubiri kwa muda mrefu lakini nataka niwaambie wananchi na Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali na lengo lake ni kulinda raia na mali zao. Tunaposikia mahali kuna majangili, kuna majambazi, kuna magaidi, kuna watu ambao aidha wanataka ama wanafanya shughuli ama mambo ya uvunjifu wa amani, sisi kama vyombo vya ulinzi na usalama wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kutuliza na ikiwezekana kukamata kila kinachohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukitazama hili jambo suala la uchunguzi sio jambo la kusema kwamba tunafanya leo na kesho na silaha zimetajwa hapa katika jibu la msingi ni karibu 1,579. Lakini hazikukamatwa silaha tu kuna wahalifu waliokamatwa na silaha hizi sio hizi silaha hizi tu kuna visu, kuna mapanga na nyinginezo. Nadhani wengi wenu mnakumbuka zile operesheni za Kibiti na nyingine.
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake waendelee kuwa na subira. Serikali kupitia vyombo tunafanya uchunguzi kuhakikisha kwamba nani anayehusika na silaha ipi inahusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ukiangalia katika masuala ya investigation sio jambo la kusema tunafanya leo, kesho tunapata majibu na ndio maana watu wengi walilalamika jambo linachukua muda mrefu kuchunguzwa kwa sababu tunataka tutende haki.
Lakini swali la pili je, sasa Serikali ina mpango gani mbadala kusaidia kupunguza sasa hizi adha za wanyama pori. Nataka niendelee tena kumuambia Mheshimiwa Kawawa pamoja na wananchi wa Jimbo hili kwamba Serikali imekuwa ikifanya operesheni na misako mbalimbali ya kusaka hawa watu wahalifu. Lakini pia kuwasaidia kuepukana na madhara ya hawa wanyama pori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kumekuwa kuna Jeshi letu hili linaloshughulika na masuala ya wanyama pori wanaweza pia tukawasaidia kupitia hili. Vilevile Serikali tumetoa namba maalum hasa kwa wale watu ambao wanafanya kazi za kilimo na shughuli nyingine katika misitu, lengo na madhumuni ikitokea mtihani wowote waweze kutuambia. Tuendelee kuwaomba radhi na kuwaambia wananchi wasubiri jambo linafanyiwa ufuatiliaji. Nakushukuru. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved