Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dorothy George Kilave
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Temeke
Primary Question
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaajiri Walimu wa Sayansi katika Shule za Sekondari za Kata Wilaya ya Temeke pamoja na kumaliza tatizo la uhaba wa Vifaa vya Maabara kwenye shule hizo?
Supplementary Question 1
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba niongeze maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imefanya jitihada kuweza kuleta Walimu, lakini utaona kwamba, asilimia 71 ni kubwa sana kwa jimbo letu la Temeke au Wilaya nzima ya Temeke. Sasa je, Serikali haioni kwamba, inaweza kufanya jitihada za ziada ili kuweza kupata vibali kwa halmashauri zetu kuweza kuajiri Walimu kwa mikataba, hao wa sayansi ili tuone kwamba, elimu sasa inaendelea mpaka hapo Wizara itakapokuwa imepata namna ya kuweza kuajiri?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuhusiana na vifaa katika sekondari zetu, je, bado haionekani ya kwamba, tunaweza tukapata vibali hivyo tukaweza kununua vifaa hivi kwa ajili ya maabara zetu, badala ya kusubiria wadau na sisi tuna fedha katika manispaa zetu? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali imeendelea kufanya jitihada za makusudi, ili kupunguza pengo la upungufu wa Walimu wa sayansi katika shule zetu za sekondari, lakini mikataba ya ajira kwa watumishi wa umma; tayari Serikali ilishaandaa modal ya mikataba kwa halmashauri zetu kuajiri watumishi kwa mkataba kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri.
Kwa hiyo, kibali kilishatolewa na watumishi wote wa sekta ya afya, sekta ya elimu na wengine ambao halmashauri kwa uwezo wa mapato ya ndani wana uwezo wa kuwalipa mishahara kwa mikataba, kibali kilishatolewa na tunatia shime kwamba, waendelee kutumia fedha za mapato ya ndani kuajiri watumishi kwa ajili ya kupunguza pengo la upungufu wa watumishi hao.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vifaa vya sayansi kwa shule za sekondari, nalo linafanana na jibu langu la kwanza kwamba, mapato ya ndani ni sehemu ya fedha za Serikali kwa hiyo, kazi yake ni pamoja na kutatua changamoto zikiwemo za upungufu wa vifaa vya sayansi katika shule zetu. Kwa hiyo, lazima halmashauri zitenge fedha hizo ili kupunguza mapengo ya vifaa hivyo. Nakushukuru.
Name
Abdallah Jafari Chaurembo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Primary Question
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaajiri Walimu wa Sayansi katika Shule za Sekondari za Kata Wilaya ya Temeke pamoja na kumaliza tatizo la uhaba wa Vifaa vya Maabara kwenye shule hizo?
Supplementary Question 2
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ina upungufu wa Walimu 6,300. Je, Serikali haioni haja ya kuleta Walimu wapya kujaza nafasi zote za Walimu waliofariki na kustaafu wa Manispaa ya Temeke?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo Abdallah, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, watumishi wetu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na maeneo mengine ya Serikali, wale ambao kwa sababu moja ama nyingine wanastaafu ama kufariki dunia, utaratibu wa kujaza nafasi zao unafuata utaratibu wa ajira za kawaida, lakini kwa kuzingatia uhitaji katika halmashauri husika.
Kwa hiyo, wale watumishi ambao katika Halmashauri ya Temeke wamestaafu, wanafahamika idadi yao, lakini waliofariki idadi yao inafahamika na wakati wa vibali vya ajira moja ya maeneo ambayo yanawekewa kipaumbele ni kujaza nafasi hizo. Nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved