Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Eng. Stella Martin Manyanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nyasa
Primary Question
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: - Je, kwa mwaka 2018 hadi 2021 ni walemavu wangapi wenye sifa husika wameajiriwa katika nafasi zilizotolewa na Serikali, na ni sawa na asilimia ngapi ya watu wenye ulemavu wenye sifa hizo nchini?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na shukrani kwa majibu hayo yenye matumaini, na ninaamini kwamba nitaweza kupatiwa orodha ya hao walioajiriwa na maeneo waliyoajiriwa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamu, hiyo kanzidata inafanya vipi kazi yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa ameeleza kwamba wanaajiriwa kwa kufuata usawa kwa watu wote, lakini mtu mwenye changamoto ni tofauti na mtu mzima. Kwa nini Serikali sasa isifikirie kuweka utaratibu maalum unaolihusu kundi hili ili lisipate tatizo kama ambavyo tunasikia kuna matatizo? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameuliza kama kanzidata ipo. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge ambaye amekuwa mstari wa mbele vilevile kulifuatilia hili suala, kwamba kanzidata hiyo ipo na inaratibiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Na katika kuratibu huko Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikitoa elimu mbalimbali kwa watu wenye ulemavu kupitia vyama vya watu wenye ulemavu, kupitia taasisi za elimu ili kuwaonesha kwamba kanzidata hiyo ipo na taarifa zao zinachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili, kwamba kwa nini kusiwe na utaratibu maalum; utaratibu maalum upo. Kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, kifungu Na. 5(1)(1) na kifungu Na. 5(1)(2) kimeeleza wazi hii sheria ya mwaka 2008, imeeleza wazi namna ya kuweza kupata ile asilimia tatu ya watu wenye ulemavu katika utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nirejee tena kutoa rai yangu kwa watu wenye ulemavu na kwa waajiri wote, kwamba watu wenye ulemavu kwanza waombe hizi nafasi zinapotangazwa. Kwa sababu kwa mujibu wa sheria asilimia ile tatu ipo lakini ni lazima wafikie sifa na vigezo vya kuajiriwa katika utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili, vilevile ni waajiri wenyewe kuwapa kipaumbele hawa watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha wakati wa interviews hizi kuwe kuna mazingira rafiki ya kuweza kuhakikisha wanahudhuria interviews hizi, wanafanya mitihani hii ambayo inawekwa ili kuweza kupata ujumuishaji zaidi wa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: - Je, kwa mwaka 2018 hadi 2021 ni walemavu wangapi wenye sifa husika wameajiriwa katika nafasi zilizotolewa na Serikali, na ni sawa na asilimia ngapi ya watu wenye ulemavu wenye sifa hizo nchini?
Supplementary Question 2
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kuuliza swali dogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tamko ambalo limetolewa na Waziri wa TAMISEMI kuomba kibali cha ajira za watumishi 7,000 walimu. Na kwenye nchi hii tuna walimu wengi wanaojitolea kufanya kazi bila kulipwa. Kule Makete nina watumishi karibia 100 ambao ni walimu wanaojitolea; je, ni upi mpango wa Serikali kuwapa kipaumbele walimu hawa au wafanyakazi hawa ambao wameonesha moyo wa utayari na uzalendo wa kufanya kazi bila malipo na wanakwenda kuomba ajira? Naomba majibu ya Serikali. (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Richard Tuntemeke Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Bungeni Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, alishatoa kauli ya kuwaagiza waajiri wote kwa maana ya wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali nchini, kuhakikisha wanafikisha majina ya watu wote wanaojitolea katika sekta ya afya na katika sekta ya elimu ili iwekwe katika kanzidata yao katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili waangalie utaratibu bora wa kuweza kuwaingiza katika utumishi wa Umma pale ajira zinapotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nirudie kauli ile tena ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ya kuwataka wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha majina ya wanaojitolea walimu shule za msingi na sekondari, wale wauguzi na katika sekta ya afya kwa ujumla wawasilishe majina hayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili utaratibu huo maalum unaoangaliwa uweze kufanyika kwa haraka wakati majina hayo yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitoe angalizo; katika kuleta majina hayo watende haki. Walete majina ya wale ambao wamejitolea kwa muda mrefu, wasilete majina ya watu ambao huenda amesikia kauli hii anakwenda kujitolea kesho na anataka jina lake na yeye liweze kuingizwa. Waangaliwe wale waliojitoa kwa muda mrefu na tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI kuona namna bora ya kuweza kuwaingiza katika utumishi wa Umma. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved