Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ng'wasi Damas Kamani
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia Balozi zetu kuhakikisha Vijana wengi wa Kitanzania wanaajiriwa nje ya nchi?
Supplementary Question 1
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Hivi karibuni nchi jirani ya wenzetu imeingia makubaliano na nchi za uingereza za kupeleka wataalam wa afya vijana kwa ajili ya kufanya kazi kule. Majibu ya Serikali ni mazuri, lakini matokeo yake hayaridhishi. Ni lini hasa Serikali itaona haja ya kuja na mikakati mbadala ya kuhakikisha inatumia Balozi zetu tulizonazo katika nchi zaidi ya 25 na Balozi Ndogo kwenye nchi zaidi ya 15 kuhakikisha inaongeza mawanda ya vijana kupata ajira? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mheshimiwa Rais wa nchi yetu, Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya juhudi kubwa sana za kuhakikisha anapanua mawanda ya mahusiano ya Kimataifa kwa nchi yetu katika nchi za Kimataifa, lakini takwimu zinaonesha kwamba, vijana wachache sana wanapata nafasi za ajira kwenye nchi jirani. Serikali je, inalitambua hili? Na kama inalitambua ni lini hasa itaanza kuchukua hatua ili kuhakikisha juhudi za Mheshimiwa Rais zinapata tija ya ajira kwa vijana? Ahsante. (Makofi)
Name
Amber. Mbarouk Nassor Mbarouk
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna haja ya Serikali yetu kuongeza juhudi katika kuhakikisha kwamba, vijana wetu wanapata fursa za ajira nje ya nchi. Miongoni mwa mbinu hizo ni kuhakikisha kwamba, tunaingia mikataba na nchi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, fursa zilizopo huko zinapatikana.
Mheshimiwa Spika, mfano hivi sasa tayari tumeshaingia mkataba na nchi ya Qatar mwezi uliopita tu ujumbe mkubwa wa Tanzania ulikwenda Doha mahsusi kwa ajili ya kufuatilia mkataba huo. Katika makubaliano yao tayari nchi ya Qatar imekubali kufungua Visa Centre hapa Tanzania maalum kwa ajili ya vijana wa Tanzania kwenda kufanya kazi Qatar. Pia tumeanza mazungumzo na nchi za Falme za Kiarabu na Oman na Saudi Arabia kwa ajili ya kuingia nao mkataba. Hii mikataba ni muhimu sana kwa sababu ndiyo inayotupa uhakika wa kupata hizo ajira.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba, Serikali imeona kuna umuhimu mkubwa sana wa vijana wetu kupata ujuzi kabla ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi. Hivyo basi, kupitia TAESA ambao ni wakala maalum wa taasisi ya ajira hapa Tanzania, imeanzisha kanzi data na ina portal maalum ili vijana waweze kujiandikisha mara zinapotokea fursa za ajira waweze kuajiriwa.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tayari portal hiyo ina vijana wanaofika 40,000 na umuhimu wake ni kwamba, hao vijana kabla ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi huwa wanapewa mafunzo maalum ili kuhakikisha kwamba, wanapokwenda huko nje hawaharibu katika kazi ambazo wamepelekewa. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved