Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Albert Ntabaliba Obama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Primary Question

MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa barabara ya Mnanila – Kasulu yenye urefu wa kilometa 42 kwa lami. (a) Je, lini barabara hiyo itaanza kujengwa? (b) Zile kilometa nne ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba zingeanza kujengwa kwa kiwango cha lami katika Makao Makuu ya Wilaya ya Buhigwe utaanza lini?

Supplementary Question 1

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwanza nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Buhigwe, kupongeza Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi. Kwanza pongezi zimuendee Mheshimiwa Rais mwenyewe, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kuikazania barabara hii alipokuwa Waziri wa ujenzi. Lakini niendelee kupongeza Wizara ya TAMISEMI, nayo imechukua juhudi hiyo ili iweze kujengwa. Lakini naomba nimpongeze tena Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuiweka kwenye mpango barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali moja dogo la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye Jimbo letu na Wilaya yetu ya Buhigwe makao makuu ya Wilaya yamebadilika kutoka Kasulu kwenda Buhigwe lakini tunazo barabara nyingine ndani ya Halmashauri yetu ambazo inabidi zichongwe kwa ajili ya kufika makao makuu na kupunguza urefu wa kuzunguka. Tunazo barabara kama nane ambazo zinahitaji kama shilingi milioni 950. Naomba ushauri wako.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukiweka rekodi sawa, Mheshimwa Obama toka kipindi chote cha miaka mitano ambapo alikuwa kama partner wangu wa karibu zaidi alikuwa akizungumzia maeneo haya ya barabara zake na amefanikiwa kuhakikisha kwamba wamehamisha makao makuu. Lakini nikijua wazi kwamba Sera ya Barabara tunaanza kipaombele katika zile barabara za kwanza zilizokuwa bora zaidi. Maana sera ya barabara ndiyo ilivyo hivyo; zile barabara ambazo hazijafunguliwa zinapewa kipaumbele cha mwisho zaidi.
Mheshimiwa Mweyekiti, sasa kwa sababu barabara hii kwa jinsi Mheshimiwa Mbunge alivyouliza ni barabara mpya, lengo ni ku-connect vizuri, kurahisisha ule umbali uwe mfupi zaidi. Nimsihi Mheshimiwa Mbunge, hili ni jambo jema, wananchi lazima wapate huduma, lakini nipende kuwahamasisha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo mumuunge mkono Mbunge huyu sasa katika vile vipaumbele vya kufungua barabara hizo mpya; kwa sababu hii ni barabara ya ndani ya Halmashauri, jambo hili katika Kamati ya Uchumi hali kadhalika katika Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani muangalie jinsi gani sasa mtatumia own source japo angalau kuanza kulifungua. Ofisi ya Rais TAMISEMI katika suala zima la kufungua barabara zake za vikwazo tutaangalia jinsi gani kwa njia moja au nyingine zile Halmashauri za pembezoni zote ambazo zina changamoto kubwa za miundombinu ya barabara tutaziangalia kwa jicho la karibu ili wananchi waweze kupata huduma za kijamii katika maeneo yao.

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa barabara ya Mnanila – Kasulu yenye urefu wa kilometa 42 kwa lami. (a) Je, lini barabara hiyo itaanza kujengwa? (b) Zile kilometa nne ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba zingeanza kujengwa kwa kiwango cha lami katika Makao Makuu ya Wilaya ya Buhigwe utaanza lini?

Supplementary Question 2

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa sera zinaelekeza kwamba barabara zinazounganisha mikoa zitajengwa kwa kiwango cha lami na kuna barabara inayotoka Mbulu kuja Karatu kwa maana inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara, ni barabara ya siku nyingi; ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera zetu nimezieleza wazi, sera hizo zinatafsiriwa vizuri katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Na Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema itawafikia wananchi wote hasa kuunganisha hii mikoa. Kama eneo hili linaunganisha Mkoa kwa Mkoa, Waziri wa Miundombinu akifika katika hotuba yake hapa nadhani atatuelezea mchanganuo wa mambo mengi zaidi. Kikubwa zaidi ni kwamba katika utekelezaji wa Ilani, maeneo yote yaliyoainishwa kwamba yatafikiwa, kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, jambo hilo litafanyika.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kesho tuna bajeti yetu, na barabara zote ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami tutaeleza kwa kina kesho. Naomba Waheshimiwa Wabunge muwe wavumilivu mpaka kesho mtasikia mambo yote. Ahsanteni.