Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Selemani Moshi Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Primary Question
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Vijiji vingi katika Jimbo la Mpanda Vijijini havina huduma ya umeme. Je, ni lini Serikali itapelekea huduma ya umeme katika vijiji hivyo?
Supplementary Question 1
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, mradi wa ORIO ulikuwepo toka mradi wa umeme vijijini Phase II ambao ulihusisha vijiji vitano, vya Kabungu, Ifukutwa, Igalula na Majalila. Mradi huu ulikwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha, Serikali ilishindwa kuwekeza fedha ambazo zinge-support kampuni ya ORIO. Je, Serikali ina majibu yapi sahihi ambayo yatawezesha miradi hii iweze kukamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nilikuwa nataka kufahamu uwiano wa miradi hii ya umeme vijijini. Yapo maeneo mengine ambayo sasa hivi yana asilimia mpaka 80, yamepata miradi hii, maeneo mangine bado hayajakuwa na fedha zinazopelekwa kwenye maeneo husika kama Jimbo la Mpanda Vijijini. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya mgawanyo wa fedha zinazofadhili Mradi wa Umeme Vijijini?
Name
Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Vijijini
Answer
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge, kwamba mradi wa ORIO ni wa Uholanzi. Ni kweli kwamba sisi tulikuwa hatujalipa fedha, lakini sasa fedha zimelipwa na hiyo mitambo imetengenezewa Ubeligiji na itafungwa. Ndio maana engine nyingine ambazo zilikuwa Ngara na kwingine tutahamisha, kwa sababu engine zinakuja zimeshatoka na wanazifunga kule; kwa hiyo mradi huo utatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la nyongeza juu ya uwiano, ni kweli napenda kukiri, kwanza Awamu ya Kwanza ya Umeme Vijijini, ilikuwa ni ya majaribio, ilifanyika ndani ya mkoa mmoja tu, Awamu ya Pili, tumejaribu kwenda nchi nzima. Lakini ukweli ni kwamba uwiano sio mzuri, na ndiyo maana Awamu ya Tatu tumekubaliana kwamba itabidi tufanye tathimini mkoa kwa mkoa, tuone mikoa ambayo imefaidika kwa kupata umeme Awamu ya Kwanza na ya Pili, safari hii watapata vijiji vichache kusudi vijiji ambavyo havijapata umeme vipewe kipaumbele.
Ninapenda kukiri kwamba mikoa ambayo kusema ukweli hawajapewa umeme sana ni mikoa ya Kusini Magharibi mwa Tanzania na REA Awamu ya Tatu inaweka mkazo hapo
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Vijiji vingi katika Jimbo la Mpanda Vijijini havina huduma ya umeme. Je, ni lini Serikali itapelekea huduma ya umeme katika vijiji hivyo?
Supplementary Question 2
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru, na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka mwezi Machi, REA walikuwa wamepata karibia asilimia 40 tu ya fedha za kwenda kumalizia katika REA ya Awamu ya Pili. Nilitaka kujua, mpaka sasa hivi Wizara yako imepokea kiasi gani ili vijiji vyangu ambavyo vilikuwa viporo kabla ya hii REA ya Awamu ya Tatu, kama Kunzugu, Mihale, Nyamatoke, Bukole, Kamkenga, Kangetutya, Rwagu na maeneo mengine yapate umeme katika ule ule mpango wa REA ya Pili na huu wa REA ya Tatu?
Name
Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Vijijini
Answer
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba tulikuwa asilimia 40, lakini kwa sasa hivi tuko zaidi ya asilimia 75, kwa hiyo jinsi ambavyo tunakusanya fedha na ndivyo jinsi ambavyo Hazina inatupatia fedha. Kwa hiyo, kwa mipangilio inavyokwenda na wakandarasi tumewaambia huu mwezi Mei tutafanya tena tathmini kwa kila mkandarasi amefanya kazi kiasi gani, nadhani hadi kufikia mwezi Mei tutakuwa tumefika karibu asilimia 80. Mheshimiwa Mbunge nataka kukuhakikishia na ndiyo maana tumekubaliana na ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge kama miradi yako ya REA Awamu ya Pili haikukamilika ni lazima itapewa kipaumbele kwenye REA Awamu ya Tatu.
Name
Mendard Lutengano Kigola
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Primary Question
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Vijiji vingi katika Jimbo la Mpanda Vijijini havina huduma ya umeme. Je, ni lini Serikali itapelekea huduma ya umeme katika vijiji hivyo?
Supplementary Question 3
kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Katika Mpango wa REA kwamba itapeleka umeme vijijini, kuna vijiji vya Jimbo la Mufindi Kusini vyapata karibu 30 havijapata umeme, kuna nguzo zilipelekwa kule na baadaye zile nguzo zikaenda kuhamishwa na wananchi wana wasiwasi. Mheshimiwa Waziri naomba uwathibitishie wananchi kwamba kwenye mpango huu wa tatu wanaweza kupata huo umeme?
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika maeneo ya Mufindi kuna nguzo zilipelekwa na mashimo yakachimbwa, lakini kutokana na scope ya kazi ile ilionekana kwamba mashimo yalikuwa yamechimbwa maeneo ambayo siyo yenyewe. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu, tumeshakaa na Mheshimiwa Mbunge, tumetathmini vijiji vyake vyote vya Mufindi Kusini na vyote alivyoviorodhesha vitaingia kwenye REA III na vitapatiwa umeme kwenye REA III inayoanza mwezi Julai mwaka huu.
Name
Rev. Peter Simon Msigwa
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Iringa Mjini
Primary Question
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Vijiji vingi katika Jimbo la Mpanda Vijijini havina huduma ya umeme. Je, ni lini Serikali itapelekea huduma ya umeme katika vijiji hivyo?
Supplementary Question 4
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa pesa ambazo MCC walikuwa waipatie Tanzania zingeshiriki kutatua tatizo kubwa na kero kubwa ya umeme na sasa wamesitisha kutoa pesa hizo. Je, Serikali inaweza kutuambia ni athari gani zinaweza kupatikana kwa wananchi kwa kukosa msaada huo wa MCC?
Name
Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Vijijini
Answer
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote wasikilize kwa makini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna hata dola moja, hata senti moja ya MCC ilikuwa iko kwenye Miradi ya Umeme Vijijini. Hiyo hawezi kunibishia Mheshimiwa Msigwa kwa sababu mimi mwenyewe ndiyo nimeenda kukaa na watu wa MCC, nimekaa na Waziri wa Nishati na wa Fedha wa Marekani, hizo fedha zilikuwa haziji Bungeni hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la MCC halafu fedha zote za MCC hazikuwa za umeme vijijini. Hilo nalo ni kosa lingine ambalo lazima watu waelewe, kuna fedha za barabara halafu kuna fedha za maji na vitu vingi sana, katika zile fedha za MCC zilizokuwa za umeme hazivuki theluthi moja. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania ni kwamba mimi tunaongea kwa takwimu, siyo ubishi, ni takwimu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote naomba hili jambo tulielewe hivi, mimi hapa ninataka kulima heka nane za mahindi, ndugu yangu, rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango anasema Mheshimiwa Muhongo kwa nini ulime heka nane? Mimi naomba nikuongezee heka mbili, ili zitimie ziwe kumi na mimi nasema ahsante ndugu yangu nipatie. Kwa hiyo, asiponipatia hizo heka mbili mimi bado za kwangu nane nitalima.