Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mariamu Nassoro Kisangi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza: - Je, nini mpango wa kuhakikisha Madereva wa magari ya abiria na mizigo wanapewa mikataba ya kazi ili kupata mafao na Bima za Afya?
Supplementary Question 1
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa madereva wengi wamekuwa wakifanya kazi na kupata ajali lakini na matatizo mengine ya kiafya hali ambayo wanakuwa mzigo kwa familia. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia hawa madereva waweze kupata haki zao za msingi kuepukana na vifo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tamko limetolewa muda mrefu na mpaka sasa kuna baadhi ya wamiliki wa magari hayo hawajatoa mikataba hiyo. Je, nini tamko la Serikali kuhusiana na hilo?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza Mheshimiwa Kisangi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, madereva ambao wanaopata ajali au maafa kutokana na kazi ambazo wanazifanya, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao unawajibika na kuhakikisha kwanza maeneo yote rasmi ya waajiri yanasajiliwa na kutoa michango kwa ajili ya fidia pale mfanyakazi anapopata madhila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo Sheria ya Workers Compensation ambayo nayo pia inahusika na masuala ya ulipaji fidia. Sambamba na hilo Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko na maboresho kwenye sheria za bima ambapo vyombo hivi vinakatiwa bima na zipo bima ambazo zinawa-cover pia wale ambao watapata madhila kutokana na ajali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Kisangi ameuliza kuhusu waajiri ambao hawajatoa mikataba. Naomba nitoe tamko rasmi la Serikali kama jinsi alivyonitaka nifanye, tamko rasmi ni kwamba, ni kosa kisheria kama umeajiri mfanyakazi na haumpatii mkataba, kwa sababu sheria zinatoa maelekezo, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, inatoa haki za mfanyakazi, lakini pia wajibu wa mwajiri. Wajibu wa mwajiri unaelezwa katika sheria hiyo zikiwa ndiyo haki za mfanyakazi. Kwa hiyo, ina reciprocate kwamba haki za mwajiri, ndio wajibu wa mfanyakazi na wajibu wa mfanyakazi ndio haki za mwajiri. Kwa hiyo, mtu yoyote ambaye hatatoa mkataba wa kazi na maeneo hayo tumekuwa tukiyabaini, tumekuwa tukiwachukulia hatua na ikibidi kuwapeleka mahakamani ili waweze kutekeleza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe rai kwa maeneo yote Watanzania wanaonisikiliza lakini pia Waheshimiwa Wabunge, kama kuna maeneo ambayo tuna uhakika kwamba hawatoi mikataba ya kazi pamoja na kaguzi zetu mtupe taarifa ili tukachukue hatua stahiki kwa wakati unaostahili. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved