Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mohammed Said Issa
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Konde
Primary Question
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wigo wa biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara ili kuongeza mapato?
Supplementary Question 1
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyonipatia kwenye swali langu hili la msingi, maswali yangu ni kama ifuatavyo.
Kwa vile amesema kwamba Serikali ina mpango wa kuondosha vizuizi vya biashara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuviunganisha vyombo ambavyo vinazuia biashara kuwa na kasi kwa mfano, ZBS na TBS kuweza kuunganika na ikiwa mzigo umekaguliwa Zanzibar iwe imetosha ama mzigo ikiwa umekaguliwa Tanzania Bara iwe imetosha. (Makofi)
Swali la pili, kwa vile tunataka kuongeza mapato ya wananchi pamoja na Serikali; Je, sasa Wizara yako haioni ni wakati wa kukaa na Wizara ya Fedha ili kuiruhusu biashara kufanyika wakati wa siku za Jumapili kama zilivyo border nyingine ambazo zinafanyakazi siku Saba kwa wiki? (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Said Issa Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli moja ya mikakati ambayo tunaiweka ni kuona namna gani tutaboresha kwa kuunganisha baadhi ya taasisi ambazo zinafanyakazi zinazofanana kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo hizi za ZBS na TBS. Lakini kwa sababu haya ni mambo ya Kimuungano naomba tuendelee kuyafanyia kazi ili tuweze kuona namna gani tutaendeleza mashirikiano kati ya mamlaka hizi mbili na mamlaka nyingine ambazo zinashirikiana katika kufanyakazi zinazofanana kati ya pande hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kweli moja ya vitu ambavyo tunavifanya katika kuhakikisha tunaongeza mapato ni kuboresha au kurahisisha ufanyaji biashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara. Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara tunachukua ushauri huu ili tuweze kuona namna ya kukaa na wenzetu Wizara ya Fedha na Mipango kuboresha siku ambazo ni za sikukuu au Jumapili au weekend ambazo wakati mwingine kunakuwa na changamoto ya ufanyajikazi ili tuweze kuwahudumia wafanyabiashara vizuri waweze kufanya shughuli zao katika siku hizi za weekend.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved