Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Primary Question
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:- Mkoa wa Simiyu ulianzishwa kisheria na Makao Makuu yake kuwa kwenye Mji Mdogo wa Bariadi badala ya Mji wa Maswa:- (a) Je, ni vigezo gani vilitumika kuamua Makao Makuu ya Mkoa na shughuli zake yawe Bariadi badala ya Maswa ambako kuna majengo ya kutosha ya Serikali; badala yake Serikali inaingia kwenye matumizi makubwa ya kupanga ofisi toka nyumba za watu binafsi huko Bariadi? (b) Je, Serikali inaweza kufikiria kubadilisha maamuzi haya kwa manufaa ya Taifa?
Supplementary Question 1
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kujua ushirikishwaji wa vikao vya Wilaya ya Maswa, kwa sababu jibu lake la mwanzo ameeleza kwamba vijiji vilishirikishwa, lakini nina hakika kabisa ushirikishwaji wa vijiji hivi na Kamati hizi zilizoorodheshwa hapa sina hakika navyo. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuniridhisha kwa kunionesha vikao hivi vilifanyika lini na wapi ili watu wa Maswa waweze kulitambua hilo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mwenyekiti wa RCC ni Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa wakati ule alikuwa ni Dkt. Balele ambaye naye anatokea Bariadi, huoni naye alikuwa labda ni sehemu ya kufanya Serikali iingie kwenye matumizi makubwa, kupeleka sehemu ambapo hakuna majengo mengi ikilinganishwa na Maswa ambayo ni Wilaya kongwe iliyozaa Bariadi na Meatu?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya awali, kwa sababu suala la michakato ya kuanzisha Wilaya, kuanzisha Halmashauri, kuanzisha Mkoa mpya yote haya hayaanzii katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, haya ni maoni ya wadau ambao wameona kwamba kuna haja ya kufanya hivyo, wanakaa katika vikao halali na kufanya maamuzi.
Mheshimiwa Spika, nimesema pale awali kwamba kikao hiki kilipitishwa na wajumbe, tarehe 10 Mei, ndiyo walifanya maamuzi hayo. Sasa nikisema nirejee kuthibitisha vikao kwa sababu suala hili nadhani DCC zote kabla hujafika katika maeneo mbalimbali; kuna vikao vya Mabaraza ya Madiwani, kuna Vikao vya Ushauri vya Wilaya, then kuna Vikao vya Ushauri vya Mkoa.
Kwa hiyo, nasema kwamba tukitaka kupata reference vizuri, tunapokutana katika RCC yetu inayokuja hapo tuitishe mihtasari ambayo ilipitisha, haya naamini tutayaona na ninyi ni wajumbe wa Kamati ya RCC. Kwa hiyo nadhani hili halina shaka.
Mheshimiwa Spika, suala la kusema kwamba Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa lakini asili yake alikuwa anatokea Bariadi. Naomba niwaambie ndugu zangu, tunapofanya maamuzi siku zote tusisukumwe na maamuzi ya mtu mmoja. Mimi kwa akili yangu siamini kama mtu mmoja ataburuza Kamati yote ya RCC na Wilaya yote na yakafuatwa maamuzi yake. Kikubwa zaidi tunapojipambanua katika mikutano yetu ni lazima tuwe imara kujenga hoja kujua jambo hilo linafanyika vipi.
Naamini kama kulikuwa na upungufu RCC yenu mtakaa na kufanya maamuzi sasa kwa mujibu wa sheria. Jambo hili bahati nzuri watu walileta pingamizi, lakini kutokana na vigezo vilivyoletwa, pingamizi lile baadaye ikaonekana kwamba kwa sababu maamuzi hayo yalifanyika halali kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 145, kurudisha madaraka kwa wananchi, ikaonekana ni halali. Ndipo jambo hili limekuja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ikaona kwamba ni sawa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge najua kwamba hoja yake ina msingi, lakini inawezekana wakati huo yeye hukuwepo katika RCC, lakini wenzake waliokuwepo kipindi hicho waliona kwamba jambo hilo lifanyike hivyo. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved