Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Primary Question

MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:- Wakulima wengi wa Wilaya ya Chemba wamefukuzwa katika mashamba yao Wilayani Kiteto licha ya kufuata taratibu na kudaiwa kuwa eneo hilo ni hifadhi. Je, Serikali ipo tayari kufuta uamuzi uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara wa kuwazuia wakulima hawa ili kuondoa mgogoro huu wa muda mrefu?

Supplementary Question 1

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba unisamehe tu, maswali yangu yatakuwa marefu kidogo kwa mara ya kwanza katika historia yangu ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, nafahamu kabisa Mheshimiwa Naibu Waziri anachosema humu ndani ni majibu aliyoandikiwa kutoka huko huko kwenye matatizo, waliomwandikia ndiyo chanzo cha mgogoro huu. Sasa swali la kwanza; je, yuko tayari kwenda mwenyewe badala ya kusubiri majibu anayoandikiwa kutoka huko Kiteto?
Swali la pili, hivi sasa wapo wakulima kutoka Chemba, Kongwa, Kondoa na maeneo mengine ambayo wafugaji wameamua kwenda kuchunga mashamba yao wakati yakiwa na mazao shambani na hakuna chochote kinachofanywa na mamlaka ya utawala wa Kiteto. Je, kama ninyi Waheshimiwa Mawaziri mmeshindwa kutatua tatizo hili, mko tayari sasa kuturuhusu tumwombe Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli akamalize tatizo hili?

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini kwamba majibu haya tumeandikiwa na hao hao ambao wamesababisha mgogoro huo ni tuhuma nzito na nataka nikubaliane na ombi la Mheshimiwa Mbunge la kwenda kuuona ukweli ukoje sisi wenyewe. Kwa hiyo, tutajitahidi, tutajipanga ili tuweze kwenda. (Makofi)
Pili, ni kwamba migogoro ya ardhi nchini ya mwingiliano kati ya shughuli za kilimo na shughuli za ufugaji inachochewa sana na maendeleo, kwamba wananchi sasa kila mmoja anatafuta namna ya kupata maendeleo. Hivyo sidhani kama kuna namna ya muujiza unaoweza kufanyika kuimaliza kama tu wadau wote, Serikali, wakulima, wafugaji, hawatatumia busara na hekima zilizokuwa zinatumika na wazee wetu wa zamani wakati hakuna hata sheria nyingi kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika, kuthamini mali ya mtu mwingine ni jambo jema sana. Kinachotokea sasa hapa ni watu kuacha maadili na utaratibu wa kimila na desturi zetu. Zamani huko ilikuwa migogoro kama hii wanaimaliza kule, lakini unapokwenda kule unakuta kuna makundi na wanaochangia wengine ni sehemu ya watu wanaotakiwa kutatua migogoro hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sitaki nibishane na Mheshimiwa Mbunge hapa, ninachosema kesi zinatofautiana kati ya kesi moja na kesi nyingine, tutajaribu kwenda na tutakapokwenda tutajaribu kutatua tatizo hili kwa mazingira yake na kwa namna lilivyo.
Mheshimiwa Spika, lakini kusema ukweli, nikiri na nikubali kwamba liko tatizo kubwa na ni lazima sisi Serikali tulishughulikie na tuko tayari kufanya hivyo na nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitakapokwenda huko nitajaribu kushughulikia tatizo hili kwa namna lilivyo, bahati nzuri nalifahamu sana.

Name

Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Primary Question

MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:- Wakulima wengi wa Wilaya ya Chemba wamefukuzwa katika mashamba yao Wilayani Kiteto licha ya kufuata taratibu na kudaiwa kuwa eneo hilo ni hifadhi. Je, Serikali ipo tayari kufuta uamuzi uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara wa kuwazuia wakulima hawa ili kuondoa mgogoro huu wa muda mrefu?

Supplementary Question 2

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Migogoro ya ardhi hasa ya WMA imekuwa ya muda mrefu katika nchi yetu. Jimboni kwangu vipo vijiji ambavyo vina migogoro ya WMA wakati vijiji hivyo ardhi hiyo ni mali yao, lakini kumekuwa na tatizo la wakulima kusumbuliwa, kufukuzwa, kuchomewa nyumba kwenye maeneo yao. Je, ni lini Serikali itakomesha tabia hii ya kuwachomea wananchi kwenye Vijiji husika vya Kabage, Sibwesa, Kapanga na eneo la Kagobole?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, tukifanya rejea ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi katika majibu yake alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Juma Nkamia, alisema kwamba ni maeneo mbalimbali. Hata hivyo, katika suala la kutaka Wabunge kuuliza swali la nyongeza, Wajumbe wengi wamesimama kuonesha kwamba jambo hilo linagusa siyo sehemu ya Mheshimiwa Kakoso peke yake au sehemu ya Mheshimiwa Nkamia peke yake isipokuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, tukifanya rejea, Waziri Mkuu alipokuwa akitembelea katika Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine katika Kanda ya Ziwa, alipofika kule Geita miongoni mwa matatizo yalikuwa ni ya wakulima na wafugaji hasa sehemu za hifadhi.
Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu alitoa maelekezo katika Wizara ambazo kwa njia moja au nyingine zinashirikiana hasa Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maliasili na Utalii hali kadhalika na TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, naomba, Mheshimiwa Kakoso, sitaki kuweka commitment hapa ambayo maelekezo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshayatoa ni kwamba, timu itaundwa kuangalia maeneo yote ya mgogoro na kuangalia mbinu gani ya kuweza kutatua case by case kutoka na hali halisi ya mgogoro husika.
Mheshimiwa Spika, jambo hili Mheshimiwa Kakoso tumelisikia kama Serikali, ni miongoni mwa maeneo ambayo yatajumuishwa kufanyiwa kazi kwa pamoja kuondoa migogoro hii katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naongezea majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Ni kweli kuna matatizo mengi sana katika WMAs nyingi, siyo hii tu anayotoka Mheshimiwa Kakoso. WMAs zimeanzishwa kwa mujibu wa Sheria, ni maeneo ya hifadhi ambayo yanamilikiwa na wanavijiji, kandokando mwa hifadhi za Serikali, lakini WMAs hizi zimepewa mipaka na zimepewa majukumu na mamlaka ya kumiliki maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, nadhani Wilaya au kwa makusudi au kwa kutokujua wanaingilia mipaka hiyo. Kwa sababu wanaotakiwa kusimamia kuweka mipaka ya WMAs hizi ni Viongozi wa Wilaya. Sasa nitashangaa Viongozi wa Wilaya kuingia kuchoma! Hata hivyo, kinachotakiwa Mheshimiwa Kakoso hapa, kila WMA iweke matumizi bora ya ardhi katika eneo lake wanalomiliki ili ijulikane wazi sehemu ya kilimo ni ipi na sehemu ya mifugo ni ipi na mipaka hiyo na ramani hizo zinasajiliwa kwenye ngazi zote kuanzia Wilaya, Mikoa na Wizara ya Maliasili.
Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Kakoso arudi kule akaangalie je, mipaka hii ya WMAs imesajiliwa katika ngazi zote hizo na mipango ya matumizi bora ya ardhi imefanyika? Kwa sababu ikifanyika mipango ya matumizi bora ya ardhi na wanaofanya ni watalaam wa ardhi na viongozi wa Wilaya haitatokea hata siku moja kuwa na contradiction kati ya Viongozi wa Wilaya na WMAs.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, tumekusudia kama Serikali wote kwa pamoja, Wizara ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI, Maliasili na watumiaji wakubwa wa ardhi kilimo na mifugo, kukaa pamoja, kuainisha migogoro yote hii hata hiyo migogoro ambayo inasababishwa na hifadhi, wafugaji na wakulima ili kwa pamoja tukae tuweze kuitatua migogoro hii.
Mheshimiwa Spika, najua hapa wakisimama, kila mmoja ameguswa na migogoro kama hii. Kwa hiyo, ni kweli kwamba tumeamua kama Serikali tutakaa pamoja na nitaleta kwenye bajeti yangu sehemu ya migogoro kwa uchokozi, ambayo mmeshatuletea Waheshimiwa Wabunge, kama bado mingine ipo tutaendelea kujazilizia ili Wizara hizi zote zinazohusika tuweke utaratibu wa namna ya kupitia mgogoro mmoja baada ya mwingine ili tuweze kuitatua.