Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Agnes Elias Hokororo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kumaliza tatizo la maji safi na salama Wilaya za Newala, Tandahimba na Nanyumbu Mkoani Mtwara?
Supplementary Question 1
MHE. AGNES J. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022, idadi ya watu imeongezeka: Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mawanda ya mradi huo ili kuongeza idadi ya watu watakaonufaika na mradi huo?
Mheshimiwa Spika, pili, chanzo cha maji cha Chiwambo na Maratu havitoi maji kwa sasa kutokana na deni kubwa la bili ya TANESCO. Serikali ina mpango gani wa kusimamia jambo hili ili kuwawezesha wananchi hao kupata maji safi na salama?
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Answer
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Hokororo kutokana na kazi kubwa anayoifanya hasa kupigania wananchi wake kwa ajili ya kupata huduma hii ya maji.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Wizara ya Maji kutokana na takwimu hii ya ongezeko la watu, tumejipanga kutumia kwanza vyanzo toshelevu kwa maana ya mito na maziwa ili kuhakikisha kwamba tunawafikia watu wengi ili kuendelea kutoa huduma ya maji. Mathalani, huu Mradi wa Nanyumbu, tunatoa maji ya Mto Ruvuma ili kuhakikisha wananchi wengi wanaenda kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ipo mamlaka ambayo ina deni na TANESCO. Namwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge tukae ili kuona namna gani tunaweza kuisaidia mamlaka hiyo kwa haraka ili huduma iendelee kwa ajili ya upatikanaji wa maji.
Name
Anne Kilango Malecela
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Primary Question
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kumaliza tatizo la maji safi na salama Wilaya za Newala, Tandahimba na Nanyumbu Mkoani Mtwara?
Supplementary Question 2
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuitembelea Kata ya Kihurio na Kata ya Bendera na kujaribu kutatua matatizo. Mheshimiwa Waziri, nikwambie kwamba umetatua matatizo ya Kata ya Bendera, lakini matatizo ya maji kwa Kata ya Kihurio yamezidi kuwa mabaya zaidi na sasa wananchi wengine wamekuwa wakidanganywa na kupewa maneno ya kuichafua Serikali na kumchafua Mbunge: -
Je, Waziri utaniambia nini kuhusu maji Kata ya Kihurio ninapotoka mimi? (Makofi)
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Answer
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Kwa kweli nimefika katika jimbo lake na tumekwenda katika kata inaitwa Bendera, hapakuwa na mradi wa maji kabisa na tulitoa maelekezo na sasa watu wanapata maji pale Bendera. Huu ni utatuzi na Mheshimiwa Mama Anne Malecela, wewe ni mkombozi hasa katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika eneo la Kihurio, nitoe maelekezo ya haraka kwa Meneja wa RUWASA wa mkoa na timu yake, hivi tunavyozungumza kesho wawe Kihurio, nami Mheshimiwa Mbunge naomba tukae tuzungumze kwa pamoja ili tuoneshe msukumo wa pamoja kukamilisha mradi huu na wananchi waweze kupata maji.
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kumaliza tatizo la maji safi na salama Wilaya za Newala, Tandahimba na Nanyumbu Mkoani Mtwara?
Supplementary Question 3
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri na Wizara yake kwa namna anavyopambana na changamoto inayoendelea Nkasi.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayotukumba kama Taifa ni kwa sababu ya miradi tunayoitumia ni mabwawa ambayo yanategemea kupata mvua. Inapotokea mabadiliko ya hali hewa, ndiyo changamoto inaonekana kama hivi sasa.
Je, Serikali ni lini mtaanza kutumia Maziwa makuu badala ya hivi ilivyo sasa inapotokea mabadiliko tunapata changamoto? (Makofi)
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Answer
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Ni kweli sisi Wizara yetu ya Maji Mheshimiwa Rais alishatupatia maelekezo mahususi kwamba yeye ni mama, hataki kusikia wamama wa nchi hii wakiteseka juu ya adha ya maji. Wizara ya Maji itumie rasilimali toshelevu na yeye yupo tayari kutoa fedha kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanapata huduma ya maji safi na salama. Kwa hiyo, ndiyo uwelekeo wa Serikali hii ya Mheshimiwa Rais Samia Hassan kutumia rasilimali toshelevu hususan maziwa na mito mikubwa ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi.
Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Rukwa, Ziwa Tanganyika ndiyo mkombozi kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya maji. Ahsante sana.
Name
Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Primary Question
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kumaliza tatizo la maji safi na salama Wilaya za Newala, Tandahimba na Nanyumbu Mkoani Mtwara?
Supplementary Question 4
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Sengerema kuna mradi wa maji ambao unasubiri kuwekwa kwenye tangazo kwa ajili ya tender. Hili jambo limechukuwa muda mrefu sana. Sijui Waziri anasemaje mradi wa Kata ya Mabiru, katika Kata ya Igalula? Ni mradi wa siku nyingi.
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Answer
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, miradi ya maji pamoja na ujenzi wake unakuwa na taratibu zake, hasa katika eneo la manunuzi. Nataka nimhakikishie, tunakamilisha hizi taratibu, lakini huu ni mradi mkubwa na nimhakikishie, saini yake nitaishuhudia mimi mwenyewe pale Sengerema. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved