Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kavejuru Eliadory Felix
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Primary Question
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: - Je, kuna mpango gani kuweka Mazingira bora ya uwekezaji kilimo cha Michikichi pamoja na kiwanda cha kuchakata mafuta – Kigoma?
Supplementary Question 1
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa michikichi mkoani Kigoma, viwanda vidogo vidogo havitoshelezi kuchakata mafuta na bidhaa zinazotokana na zao la chikichi: Je, Serikali ina mikakati gani ya kuleta viwanda vya kati na vikubwa mkoanii Kigoma (secondary and tertiary industry)? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Serikali ina mipango gani ya kutenga maeneo ya viwanda vya kati na vikubwa katika wilaya zote za Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kavejuru Felix, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Kavejuru kwa ufuatiliaji mkubwa kuhusiana na zao la chikichi na mnyororo mzima wa thamani katika Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, ni kweli jitihada zilizopo ilikuwa ni kuanza na viwanda hivi vidogo ambavyo vilikuwa vinakidhi mahitaji wakati ule uzalishaji wa michikichi ulipokuwa katika hali ya chini kwa maana ya malighafi. Sasa juhudi kubwa zimefanywa na Serikali, tunaamini tuna malighafi ya kutosha, kwa hiyo, mipango ya Serikali sasa ni kuanza kuvutia wawekezaji wakubwa ili waweze kuwekeza katika viwanda vitakavyochakata mnyororo mzima wa thamani wa mchikichi katika Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, hii ni pamoja na kuboresha miundombinu. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba sasa tumeshapata umeme wa grid ya Taifa katika Mkoa wa Kigoma ambayo ilikuwa ni moja ya kikwazo, pia barabara zinaboreshwa ambavyo ni vitu muhimu sana kwa ajili ya kuvutia wawekezaji. Kwa hiyo, tunaendelea kuweka mazingira wezeshi na bora kwa ajili ya uwekezaji katika mikoa ya pembezoni ikiwemo Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kutenga maeneo ya uwekezaji kwenye kilimo pia na maeneo ya kujenga viwanda, kwanza nimshukuru sana kwa ushauri wake. Sisi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tunaendelea kutenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya mashamba makubwa. Pia niwaombe Serikali za Mikoa na Halmashauri ili waendelee kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji, kwa sababu hii ni endelevu, tunatakiwa tuwe na maeneo sahihi na yenye miundombinu wezeshi ili wawekezaji wakubwa wanapokuja kuwekeza viwanda hivi wasihangaike tena kupata ardhi ambayo wakati mwingine inakuwa mgogoro mkubwa kwa ajili ya kuweka viwanda hivi vikubwa.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Name
Kunti Yusuph Majala
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: - Je, kuna mpango gani kuweka Mazingira bora ya uwekezaji kilimo cha Michikichi pamoja na kiwanda cha kuchakata mafuta – Kigoma?
Supplementary Question 2
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Serikali ina mkakati gani wa kujenga kiwanda cha kukamua mchuzi wa zabibu ili kuweza kuondoa adha ya wakulima wa zabibu wa Mkoa wa Dodoma wanaotembea na mabeseni barabarani wakitembeza zabibu na kuiuza bila faida yoyote? Ahsante. (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala, kuhusiana na sekta ya kilimo hasa kwenye zao la zabibu.
Mheshimiwa Spika, tayari tumeshaanza juhudi mbalimbali za kusaidia kuchakata zabibu ili ziweze kuwa katika hali ya mchuzi wa zabibu anaosema, ambapo tayari kuna wadau mbalimbali wameshaanza kuchukua, wakiwemo kiwanda cha Jambo ambao wapo Shinyanga. Vilevile wengine wameshaanza kuchukua zabibu hizo ambazo naamini wadau hawa ambao tumewahamasisha watapunguza adha ya kutembea kuuza zabibu ambazo hazijachakatwa ambazo wakulima wenzetu wa Mkoa wa Dodoma wanahangaika nazo. Nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved