Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Khalifa Mohammed Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Mtambwe

Primary Question

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza: - Je, ni kwa kiwango gani Mbunge anashirikishwa katika miradi inayoibuliwa na wananchi katika Jimbo lake kupitia TASAF?

Supplementary Question 1

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naomba kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, niruhusu nitoe shukrani zangu za dhati sana kwa ofisi ya Rais kupitia TASAF kwa mradi mkubwa ambao wamenipelekea katika shule yangu ya Peak, kukarabati na ujenzi wa uzio shule ambayo Baba wa Mheshimiwa wetu Mzee Suluhu Hassan alifundisha, hivyo wamepeleka fedha nyingi pale nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza niliuliza Wabunge wanashirikishwaje? Nashukuru kwa majibu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati baada ya miradi ile ambayo imeibuliwa na wananchi Wabunge nao wakapata taarifa ili kuwa karibu na ile miradi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa mradi mkubwa huu uliopelekwa katika skuli ya Peak Jimbo langu la Mtambwe kukarabati madarasa na uzio kuna baadhi ya maeneo bado hayajakamilika. Je, Serikali haioni ni wakati mzuri sasa hivi wa kuweza kupeleka fedha pale ili kukamilisha baadhi ya maeneo ambayo hayajakamilika? (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khalifa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kuwapa taarifa Waheshimiwa Wabunge, naomba nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako hili kuelekeza ma-TMO wote ambao ni wasimamizi wa miradi hii ya TASAF katika Wilaya husika kuwa wanawapa taarifa Waheshimiwa Wabunge kwa miradi yote ambayo wananchi wameibua kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa tunafahamu Wabunge ndio wawakilishi wa wale wananchi wa yale maeneo husika hivyo ni muhimu sana kuweza kuwapa taarifa, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge, kwamba miradi mingine itakayoanza kuibuliwa ndani ya Majimbo husika basi Wabunge wataanza kupewa taarifa ile.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu mradi wa Peak, bahati nzuri nimefika mpaka pale, hatua ya kwanza iliyoanza kwenye shule ile ilikuwa ni kujenga madarasa ambayo yalikuwa yamechakaa sana. Baada ya kumaliza ujenzi ule wa madarasa yale, wananchi wale wa eneo lile pia waliibua mradi mwingine ambao ni hitaji lao lilikuwa ni uzio katika shule ile. Kwa sababu ilikuwa ni njia ya wakazi wa pale kukatiza katikati ya skuli ile katika eneo la Peak. Baada ya kutambua hilo fedha ikatolewa na mradi wa TASAF baada ya kuibuliwa mradi na baada ya hapo ni uzio ule umejengwa.

Mheshimiwa Spika, kama kuna hitaji jingine wananchi wanaweza wakaibua na TASAF watafanyia kazi. (Makofi)