Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Primary Question

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: - Je, ni upi mchango wa Serikali Kuu katika ujenzi wa Uwanja wa Kisasa wa Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Geita?

Supplementary Question 1

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mhehimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo Nchini. Sasa nataka kufahamu tu kwamba majukumu makubwa ya fungu hilo ilikuwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi zinazoendelea mikoani za ujenzi wa viwanja: Je, ni Shilingi ngapi ambazo Wizara inaweza kuipatia Halmashauri ya Mji wa Geita?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa Tanzania imekuwa haipati matokeo yanayoridhisha inapokwenda kwenye michezo mbalimbali nje ya nchi; na hii inasababishwa na kukosekana kwa mpango na mkakati unaopimika wa kuendeleza michezo nchini: Ni upi mpango wa haraka ambao wizara inao ili kuweza kujikwamua kwenye eneo hilo?

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naomba sasa nijibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza Mheshimiwa Kanyasu anapenda kufahamu ni kwamba Bunge hili lilitupitishia fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo na hadi sasa ni shilingi ngapi zimetumika lakini pia kama tunaweza kuwasidia Geita Mji katika ujenzi wa uwanja ule.

Mheshimiwa Spika, tushukuru Bunge hili Tukufu na Mheshimiwa Rais kwa kutupatia fedha hizi, ambazo zimetusaidia sana kwenye Timu za Taifa ambapo mmeona kwa kiasi kikubwa sana wameletea heshima Taifa letu. Sisi kama Wizara tulivyoomba fedha hizi, lengo kubwa lilikuwa ni kujenga viwanja vya kitaifa ambavyo vitasaidia vijana wetu ambao wametoka kwenye ngazi za chini kuweza kucheza kwenye viwanja vizuri. Jukumu hilo tumeanza, lakini na Halmashauri ya Geita hatujaiacha, tumewapa maelekezo mbalimbali ili waandae uwanja huu vizuri.

Mheshimiwa Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba fedha hizi zitakapokuwa zinatosha baada ya timu za Taifa kuhudumiwa, tuko tayari kuendelea ku- support jitihada hizi za Taifa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Kanyasu anapenda kufahamu ni mkakati gani Wizara yetu tumeandaa kwa ajili ya kuhakikisha tunapata wachezaji wazuri kwa ajili ya kuendeleza michezo katika Taifa letu? Kwanza Bunge hili Tukufu mlitupatia Shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya Chuo cha Malya ambacho kinatoa mafunzo kwa Makocha wetu. Pia Bunge hili Tukufu mlitupitishia fedha zaidi ya Shilingi bilioni mbili kwa ajili ya Academy 56 nchi nzima ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu amejibu hapa na fedha hizi sisi tumetenga.

Mheshimiwa Spika, vile vile tunaendelea kukarabati viwanja saba vya zaidi ya Shilingi bilioni 10 ambavyo tulivitaja hapa vikiwemo vya Mbeya, Dodoma, Arusha na maeneo mengine kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu na tunawapata wataalam kupitia fedha hizi ambazo mnatutengea.