Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha pembejeo za korosho kwa msimu wa mwaka 2022/2023 zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa miaka miwili mfululizo Serikali imekuwa ikiahidi, lakini kiasi kinachotolewa kwa ajili ya usambazaji huwa hakiendani na kile ilichoahidi, hivyo kusababisha upungufu wa pembejeo kwa wakulima. Je, Serikali inatoa kauli gani kwamba ahadi hii ya leo ya pembejeo ya unga na dawa za maji kwamba zote zitapatikana kwa wakati na zote zitafika kwa wakulima?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni ongezeko la pembejeo. Tunatarajia kwamba kutakuwa na ongezeko la uzalishaji wa korosho na tumeona pia kwenye soko la korosho bei inazidi kuporomoka. Je, Serikali ina mkakati gani kwamba ongezeko hili la uzalishaji litaendana na bei nzuri ambayo ina tija kwa mkulima wa korosho? Nakushukuru sana.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu kauli ya Serikali bahati nzuri kwenye kikao cha wadau wa korosho ambacho mimi nilikuwa sehemu ya washiriki na Waheshimiwa Wabunge walikuwepo mle ndani, tumekubaliana kwamba viuatilifu vyote na pembejeo zote ziwafikie kabla ya msimu na kwa idadi ambayo Vyama vya Msingi vitakuwa vimewasilisha katika Kamati ile ya Pembejeo. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge na kwamba Serikali itasimamia kuhakikisha viuatilifu hivi vinawafikia wakulima kwa wakati ili kuondokana na changamoto ambazo zilikuwa zinawakumba wakulima katika misimu iliyopita.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu namna ambavyo uzalishaji utaongezeka na Serikali imejipangaje katika kuhakikisha kwamba soko linakuwepo? Moja ya mkakati tulionao mkubwa ni kuhakikisha tunawawezesha wabanguaji wadogo ili kuongeza ubanguaji wa korosho ghafi na kutengeneza masoko ya uhakika ya korosho ambayo imechakatwa.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa tumeendelea kutafuta masoko nje ya nchi na wiki iliyopita mimi mwenyewe nimekwenda uwanja wa ndege kusindikiza kontena la korosho iliyobanguliwa ambayo tumepata soko Marekani na kilo moja kule inauzwa 90,000/= ambayo ni uhakika mkubwa kwa mkulima wa korosho. Hivyo mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tunawawezesha wabanguaji wadogo na kuwajengea uwezo ili tuachane kuhangaika na soko hili la Vietnam na India ambalo limekuwa na changamoto kubwa sana ya bei.