Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Venant Daud Protas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza maeneo kutoka kwenye hifadhi katika Jimbo la Igalula ili wananchi wa Igalula wapate maeneo ya kuchungia na makazi kwa kuwa idadi ya watu na mifugo imeongezeka?
Supplementary Question 1
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali ambayo yatakwenda kuzua mgogoro mwingine; katika vijiji alivyovitaja hapo ni kijiji kimoja tu ambacho kipo kwenye Jimbo la Igalula. Kuna Kamati ya Mawaziri nane ilikuja kule na ikatoa maelekezo kuwa itaenda kugawa maeneo katika maeneo haya, lakini katika jibu lake wanasema hawaoni haja.
Je, Serikali haioni sasa kuweka kauli inayoeleweka kwa wananchi ili waweze kutoa mkanganyiko ambao unajitokeza?
Swali la pili, Jimbo la Igalula limezungukwa na vijiji vingi vyenye mgogoro kama huu hasa katika Kata ya Miswaki, Loya, Igudi, Mwamabondo na vijiji vingine. Je, Serikali haioni haja ya kwenda kupitia mipaka upya ili kila mwananchi ajue ni wapi anaishia na hifadhi inaishia wapi? Ahsante.
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuhusu kauli ya Serikali iweke kauli sahihi kuhusiana na vijiji vilivyotajwa; kuna mapori matatu yapo ndani katika Jimbo la Igalula, kuna Pori la Iwembele, Uyui, Kigwa, Lubuga, kuna Nyahua.
Mheshimiwa Spika, swali la Mheshimiwa Mbunge la msingi halikuhainisha ni vijiji gani hasa ambavyo analenga. Lakini nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo la Igalula kwa maana ya Jimbo la Igalula kuna vijiji ambavyo vinaenda kunufaika na Kamati hii ya Mawaziri nane, kuna kijiji cha Miswaki, Igudi, Mwamdalaigwe, Loya na Mwamabondo, vijiji hivi vinatoka katika Jimbo la Igalula na vitaenda kunufaika na kumegewa kwa maamuzi ya Kamati ya Mawaziri nane.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuonesha mipaka, niwatoe wasiwasi Wabunge pamoja na Mbunge aliyeuliza swali kwamba kwa utaratibu tulionao sasa ni kuhakikisha kwamba yale mapori mapya ambayo tutayapa GN mpya tutaweza kushirikisha wananchi namna ya kutambua mipaka mipya na yale ambayo yatatangazwa na Serikali kwamba haya sasa ni mapori halali basi wananchi watafahamu mipaka yao ili iwe rahisi kutoingiliana tena na kuanzisha migogoro mipya.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Ardhi.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna alivyojibu swali la Mheshimiwa.
Mheshimiwa Spika, labda nijibu kwa ujumla kulingana na changamoto iliyokuwepo katika maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ameridhia kati ya vijiji 975, vijiji 920 wamekubaliwa kubaki kwenye maeneo yao. Kitakachofanyika ili kuondoa hizi changamoto ni ushirikishaji wa wananchi katika maeneo watashirikishwa wote na wataalam wote watakuwepo na katika maeneo ambayo tumekwishapita tayari wapo ili kuweza kubaini mipaka kwa pamoja. Na hii inafanyika hivyo ili baadae kusijekutokea lawama pengine kwamba hawakushirikishwa katika kubainisha mipaka mipya.
Kwa hiyo, tunaimani maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ameridhia na ameongeza hata pale ambapo alikuwa amesema kwamba wangeishia, imewapa pia fursa ya kuwa na maeneo ya akiba ya wao pia kuweza kuyawekea mpango wa matumizi ambao Serikali itafanya kwa kushirikiana na wao ili basi wasiendelee kuwa na ugomvi na hifadhi ambazo ziko zimetengwa kwa kazi maalum.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved