Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza kujenga soko la mazao la Kimataifa katika eneo la Mbimba TACRI Vwawa ili Wananchi wapate soko la uhakika?
Supplementary Question 1
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali. Ninayo maswali mawili ya nyongeza: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Bajeti ya mwaka huu Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza fedha hadi kufikia takribani shilingi bilioni 954; ni kwa nini Serikali haikuweka kipaumbele cha ujenzi wa soko hili katika hizo fedha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Songwe ni moja ya mikoa ya kimkakati, ambayo inapakana na nchi mbalimbali jirani na ambao unaongoza katika uzalishaji wa chakula, ni mkoa wa tatu kwa uzalishaji wa chakula.
Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko hili muhimu kwa wananchi wa mkoa huo? (Makofi)
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunampongeza Mbunge kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhakikisha kwamba eneo lile linapatikana kutokea TACRI. Pili, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua umuhimu wa Mkoa wa Songwe katika kilimo cha nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tutalipa kipaumbele katika bajeti inayokuja ili basi wananchi wa Mkoa wa Songwe na hasa wakulima wa mazao mbalimbali waweze kupata fursa hii ya kuwa na kituo cha mazao; na kwa sababu pia Songwe inaungana na nchi nyingine, itakuwa ni fursa ya kipekee kwa wananchi wetu kupata masoko ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalipa kipaumbele na ataona katika bajeti inayokuja.
Name
Selemani Moshi Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza kujenga soko la mazao la Kimataifa katika eneo la Mbimba TACRI Vwawa ili Wananchi wapate soko la uhakika?
Supplementary Question 2
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Serikali iliahidi kujenga Soko la Kimataifa katika Kijiji cha Itetemya, Kata ya Karema ambacho kingewasaidia kuunganisha kati ya nchi ya DRC Congo na wananchi hao: Je, ni lini huu mradi ambao iliahidi takribani miaka mitano iliyopita utatekelezwa?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilishatoa ahadi juu ya ujenzi wa soko katika eneo hilo. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi sasa kati ya maeneo ambayo tunayapa kipaumbele ni ujenzi huu wa masoko. Nimwondoe hofu kwamba katika mikakati yetu inayokuja tutaunganisha masuala ya miundombinu ya masoko tunayoyafanya na ujenzi wa masoko hayo, pamoja na kumkumbuka katika eneo lake. Hivyo Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi katika bajeti inayokuja pia tutaikumbuka katika eneo lake hilo.
Name
Oliver Daniel Semuguruka
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza kujenga soko la mazao la Kimataifa katika eneo la Mbimba TACRI Vwawa ili Wananchi wapate soko la uhakika?
Supplementary Question 3
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kuna Soko la Kimataifa lililoanza kujengwa katika Kitongoji cha Nzaza Kata ya Kabanga Wilayani Ngara 2014 na ujenzi huo ukasimama ghafla: Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi huo wa soko hilo kwa manufaa makubwa ya wananchi wa Ngara na wakulima kwa ujumla? (Makofi)
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mbunge Viti Maalumu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, soko lilopo pale Kabanga katika Wilaya ya Ngara ni kati ya masoko sita ambayo Wizara imepanga kuyamalizia katika mwaka huu wa fedha. Hivyo soko hili lipo katika mpango na litatekelezwa.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved