Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Primary Question

MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: - Je, kuna mkakati gani kudhibiti tembo wanaovamia Vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kamenyanga, Gurungu, Muhanga na Njirii?

Supplementary Question 1

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshiniwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha Doroto ambacho kimetajwa kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kituo kikubwa ambacho kinasimamia Game Reserve ya Muhesi lakini hakina gari: Je, Serikali ipo tayari sasa kupeleka gari jipya kabisa katika kituo hiki?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: kuna wananchi ambao walifariki kutokana na wanyama hao wakali katika Kijiji cha Nyabutwa katika Kata ya Mgandu na maeneo mengine mazao ya watu yaliliwa: Je, ni lini Serikali itawalipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa ajili ya kuwafariji wananchi hao kutokana na matukio hayo ya wanyama wakali?

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Omari Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshapokea magari 59 ambayo yatasambazwa kwenye vituo vilivyo na athari ya wanyamapori wakali na waharibifu, hivyo nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba priority itapelekwa katika Kituo hiki cha Doroto.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili lingine la kifuta machozi na kifuta jasho, tulikuwa na changamoto kidogo ya fedha na kufanya tathmini na tayari tumeshakamilisha. Hivyo, wakati wowote tutaanza kulipa wathirika wa changamoto hii. (Makofi)

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: - Je, kuna mkakati gani kudhibiti tembo wanaovamia Vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kamenyanga, Gurungu, Muhanga na Njirii?

Supplementary Question 2

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa napenda niipongeze Serikali na kuishukuru kwa sababu Bunge lililopita nilieleza kadhia ya tembo ambao wanawaua watu, kula mazao na kuleta uharibifu mkubwa. Naishukuru Serikali kwa kuniletea kile kituo na sasa hivi kituo kimekamilika zaidi ya asilimia 95.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, niliomba gari na askari. Gari bado sijapata na maaskari bado sijapata, lakini kitu cha kusikitisha, tarehe 6 Novemba, 2022 mwananchi wangu aitwaye Mwanahawa Mohamed Likenge ameuawa na tembo katika eneo la Lucheme Kitongoji cha Ndulima na tarehe 7 Novemba 2022 amezikwa. Sasa kwa kuwa Askari ni wachache, naomba niongezewe Askari ili waweze kufanya patrol kuhakikisha wananchi hawa wanapata manusra na hatimaye tujue hatma yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, Mbunge wa Lindi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitoe pole kwa mwananchi huyu ambaye tulipata taarifa ndani ya siku tatu kwamba ameuawa na wanyama wakali na waharibifu. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba maombi yake yote tutayatekeleza kwa wakati; na kwa kuwa tayari tumeshapata magari, basi tutayaelekeza katika eneo hilo na maeneo mengine yenye changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tumeshaanza ku-train VGS, hawa Askari wa Vijiji na tayari vijiji tisa tumeshamaliza kuwafanyia mafunzo na hawa wote watapelekwa kwenye maeneo ambayo yana changamoto hii. Tutaongeza askari katika maeneo yenye changamoto na nguvu ili kuhakikisha kwamba tunathibiti wanyama wakali na waharibifu. (Makofi)

Name

Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: - Je, kuna mkakati gani kudhibiti tembo wanaovamia Vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kamenyanga, Gurungu, Muhanga na Njirii?

Supplementary Question 3

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Manyoni ilitangaza nafasi au fursa ya kuwekeza kwenye Halmashauri yake hususan kwenye zao la korosho, lakini yale maeneo waliyoyapanga ndiyo njia kuu ya kupita tembo. Kwa hiyo, ukipanda, wakipita wanavunja, wakirudi tena wanakula yale majani. sasa nataka kujua Wizara hii lini itawasiliana na Halmashauri ya Manyoni ili wale ambao wamepata mashamba kwenye eneo lile ambalo ni njia ya tembo waweze kubadilishiwa? Ahsante. (Makofi)

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya uvamizi wa wanyama wakali na waharibifu katika mashamba ya uwekezaji yaliyoko Manyoni. Tayari tumeshaanza kuimarisha doria kwa kuanzisha usimamizi wa doria kuzunguka mashamba hayo na tuna mpango sasa wa kuweka kituo ambacho kitakuwa ni kituo cha kudumu kwa ajili ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.