Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: - Je, nini kauli ya Serikali kwa wakulima wa vitunguu maji katika Bonde la Eyasi juu ya upatikanaji wa masoko pamoja na bei ya zao hilo?

Supplementary Question 1

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Pamoja na soko kutokuwa na uhakika, kumeibuka utamaduni wa wanunuzi kufika mpaka mashambani, wao ndio wanapanga bei na aina ya vifungashio ambapo kwa kiwango kikubwa inamuumiza mkulima.

Je, Serikali inasema nini kuhusiana na hili?

Swali la pili, je, Wizara ipo tayari sasa kwenda kukaa na wakulima hawa kusikiliza changamoto zao lukuki walizonazo ili waweze kupata ahueni na kuondokana na changamoto hiyo? Ahsante. (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Paresso kwa kufuatilia hili la mazao hasa kwenye zao la vitunguu. Ni kweli kumekuwa na changamoto hiyo ya wanunuzi wengi na wakati mwingine hata wa nje kufika kwa wakulima kule vijijini. Tumeshatoa maelekezo mara nyingi hasa kwa wenzetu wa halmashauri tuendelee kushirikiana kuhakikisha tunaendelea kujenga collection centers, yaani maeneo ya kuuzia kama masoko. Maeneo hayo ndiyo maalum kwa wakulima ili waweze kuuza kwa tija na kwa vipimo.

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kusema kwamba Wakala wa Vipimo ambao wako chini yetu waendelee na waende eneo hili maalum wakaone changamoto hii iliyopo ili kukomesha ufungashaji wa mazao yetu kwa njia ambayo siyo sahihi. Maana tumeelekeza mazao yote yauzwe kwa vipimo, siyo kwa vifungashio. Pia kulikuwa na hii habari ya lumbesa, naamini tulishasema na ninarudia tena, kuhakikisha wanauza kwa vipimo na tuhamasishe halmashauri waweke collection centers ili wakulima wapate bei yenye tija kwa mazao yao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kwenda kukagua; nitaenda, na niagize WMA waende kwanza, nasi tutaenda kuona changamoto hasa katika eneo hili Bonde la Eyasi ili tuweze kutatua changamoto hii ambayo nadhani ni sehemu zote nchini na tunaendelea kufanyia kazi hilo. Nakushukuru sana.

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: - Je, nini kauli ya Serikali kwa wakulima wa vitunguu maji katika Bonde la Eyasi juu ya upatikanaji wa masoko pamoja na bei ya zao hilo?

Supplementary Question 2

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri, kumekuwa kuna shida sana ya masoko kama alivyosema kwenye swali la msingi, lakini kumekuwa na matangazo ya uwongo redio wakisema zao la vanilla linauzwa kwa kilo moja Shilingi milioni moja: Unatoa katazo gani kwa watu wanaowadanganya wakulima katika zao hili? (Kicheko)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na matangazo ambayo wakati mwingine yanaleta taharuki na hasa kwenye hili zao la vanilla kwamba linauzwa bei kubwa na wakati mwingine nadhani hii imekuwa kama zile biashara za kwenye mitandao. Kwa sababu hiyo, Serikali na kwenye maeneo mahususi kwa mfano maeneo ya Njombe, kumeshatokea utapeli huo.

Mheshimiwa Spika, tumeshaelekeza wenzetu kwenye halmashauri waone namna gani kweli hawa ambao wanadhani wanataka kusaidia wakulima, washirikiane na halmashauri kuona kweli hilo zao kama ni vanilla au mazao mengine kweli yanaweza kustahili kulimwa lakini pia kuwa na njia sahihi kuhamasisha ulimaji huo badala ya kuwa na biashara mtandaoni ambazo mara nyingi ni utapeli.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme, kwa kweli sisi kama Serikali tunaendelea kufuatilia matapeli wanaotumia biashara mtandao kutapeli wakulima au wananchi kutoa fedha ambazo mwisho wa siku haziwezi kuwa na tija kama ambavyo wamelenga. Nakushukuru.