Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Deo Kasenyenda Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Primary Question
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:- Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha Afya cha Makambako kuwa Hospitali lakini tatizo kubwa lililopo ni ukosefu wa vifaa tiba na kufanya watu wengi kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula. Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa hivyo ili watu wasipate taabu ya kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula?
Supplementary Question 1
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru majibu mazuri ya Waziri ya kutununulia baadhi ya vifaa vya upasuaji ili tupate huduma hii. Kama nilivyosema vifaa hivi vimekaa tu haviwezi kufanya kazi, ni sawa na mifugo umechukua majike umeyaweka hujapeleka madume hakuna kitu ambacho kitaendelea pale. Serikali haioni sasa uko umuhimu wa kupeleka kwa mfano hizi dawa za usingizi ili shughuli za upasuaji ziweze kuanza? (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Rais alipopita pale aliahidi kuwaondolea kero wananchi wa Makambako ili wasiende kufanyiwa upasuaji Njombe na Kibena kama nilivyouliza kwenye swali la msingi. Hawaoni sasa iko haja ya kuchukua fedha za dharura kununua vifaa hivi pamoja na vile vilivyopelekwa ili shughuli za upasuaji zianze?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deo Sanga kama ifuatavyo:-
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
13
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikiri nilifika pale Makambako na nikaenda mpaka Hospitali ya Kibena wakati nilipotembelea Makambako mpaka Njombe. Kihistoria ni kwamba watu wa Makambako walikuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Kibena na ni kweli Hospitali hii inakabiliwa na changamoto kubwa sana na nimshukuru Mbunge kwa kweli lazima niweke wazi, ni miongoni mwa Wabunge ambao kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana na nilitembelea mpaka miundombinu ambayo yeye mwenyewe alishirikiana na halmashauri yake kuiweka sambamba na miundombinu ya elimu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tunakupongeza kwa hilo kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwamba vifaa viko pale havifanyi kazi ni kweli na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema vifaa vile havifanyi kazi. Pia hata lile jengo nadhani ukarabati ulianza kufanyika na hata mfumo wa maji zile koki zenyewe zilikuwa hazifanyi kazi vizuri. Kulikuwa kunatakiwa koki maalum ambazo unagonga kwa mkono inafunguka badala ya kushika ku-avoid contamination. Zoezi hilo limeenda vizuri ikiwa ni pamoja na urekebishaji wa mitaro, lakini changamoto kubwa pale imekuwa ni fedha. Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha ile bajeti iliyotengwa iweze kufika angalau lile jengo lifanye kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia amesema wazi Mheshimiwa Rais alipita kule wakati wa kampeni na aliahidi kushughulikia hospitali ile ya Makambako ili ifanye kazi vizuri. Kuhusu kutenga pesa za dharura, mimi nasema jukumu letu kubwa katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha tunaoenda nao ile bajeti ambayo ilielekezwa kwenda pale ambayo kwa bahati mbaya haijafika vizuri basi tutawasiliana ndani ya Serikali yetu ili iweze kwenda. Sasa hivi tumesema tumeongeza sana ukusanyaji wa mapato tutahakikisha yale mapato yanayokusanywa kwa zile bajeti zilizopangwa ambazo pesa hazijapelekwa ziweze kupelekwa ili miradi iweze kutekelezeka na wananchi wapate huduma.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mzee Deo Sanga naomba nikiri kwamba tutakuwa pamoja kuhakikisha kwamba wananchi wa Makambako hasa tukijua ni center kubwa sana kwa watu wa Mbeya na Songea, tutasaidia eneo lile liweze kupata huduma bora za afya.
Name
Amina Saleh Athuman Mollel
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:- Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha Afya cha Makambako kuwa Hospitali lakini tatizo kubwa lililopo ni ukosefu wa vifaa tiba na kufanya watu wengi kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula. Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa hivyo ili watu wasipate taabu ya kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula?
Supplementary Question 2
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la afya au linalohusiana na zahanati kwa ujumla linagusa maeneo mengi katika nchi hii ya Tanzania. Mojawapo ni Zahanati ya Nduruma iliyopo katika Kata ya Nduruma, Wilaya ya Arumeru. Zahanati hii imepandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya lakini hakuna jengo la upasuaji, hakuna vifaa na inahudumia vijiji karibia kumi. Je, Waziri anatuambia nini kuhusiana na kituo hiki cha afya ambacho hakina vifaa na wananchi wanalazimika kwenda Hospitali ya Mount Meru iliyoko mkoani Arusha?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Mollel, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki moja iliyopita Mheshimiwa Amina Mollel aliniambia kuhusu zahanati hiyo ambayo imepandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya na mimi nilimpa ahadi kwamba tutafanya kila liwezekanalo, huenda kabla Bunge hili halijaisha tutafika pale Arusha kuangalia zahanati hii. Pia ameniambia mambo mengine zaidi kwamba wataalam wengine wameondoka na zahanati ile haifanyi kazi. Naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza safari yetu itakuwa palepale mimi na yeye, tutaenda pale Nduruma kuona changamoto za zahanati ile kwa karibu zaidi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wale kutoka pale kwenda Mount Meru na Arusha ni jiji linalokuwa na population inaongezeka. Ni lazima maeneo ya pembeni tuyaimarishe ili kupunguza ile referral system kwamba siyo kila mtu ugonjwa mdogo aende katika Hospitali ya Wilaya. Serikali kupitia TAMISEMI na tutakapokwenda pamoja tutahakikisha ule upungufu tunaubaini na kupanga mpango mkakati wa jinsi gani tutafanya ili kituo hiki cha afya kiwe na vifaa tiba na wataalam kiweze kutoa huduma katika maeneo hayo na kata zinazokizunguka.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved