Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kufufua kilimo cha zao la muhogo katika Mkoa wa Mtwara?

Supplementary Question 1

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; ili zao hili liweze kufufuka na kuleta tija sio kupeleka mbegu bora tu ni pamoja na kutafuta masoko mazuri nay a uhakika ili wakulima waweze kuuza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha masoko ya uhakika yanapatikana?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; sisi Mkoa wa Mtwara muhogo ukilimwa unastawi kweli kweli lakini tunashindwa kulima kwa sababu hakuna kiwanda cha kuongeza thamani ya zao la muhogo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inajenga kiwanda yenyewe ama kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza thamani ya zao la muhogo? Nakushukuru.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika swali la kwanza la kuhusu masoko hivi sasa Wizara tumeendelea kuimarisha huduma za masoko kwa kuhakikisha kwamba mazao yetu mengi tunayatafutia masoko, ili wakulima wetu wakilima kwa tija mwisho wa siku mazao yao yaweze kupata masoko ya uhakika. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja kati ya mkakati tulionao hivi sasa ni kufanya muhogo kama sehemu ya malighafi kuu katika viwanda vyetu ambavyo tumeanza mazungumzo nao kwa ajili ya kutengeneza wanga ambao hivi sasa tunaagiza karibuni tani 8,000 kwa mwaka. Kwa hiyo, tumeanza mazungumzo na viwanda vilivyoko hapa nchini kwa ajili ya kufanya muhogo kama malighafi ya utengenezaji wa wanga. Zoezi hilo linakwenda vizuri na mwitikio umekuwa mkubwa na ndio maana sasa tumeendelea kuhamasisha wakulima wengi zaidi kulima muhogo.

Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusu viwanda. Ni kweli mwisho wa siku kama Wizara katika mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba tunaongeza thamani ya mazao yetu na kwa upande wa muhogo viko viwanda ambavyo mwanzoni vilionesha nia ya kuanza kufungua katika upande wa kule Kusini. Kwenye Kijiji cha Malamba katika Jimbo la Mtama ipo kampuni ambayo ilifungua kiwanda, Kampuni ya Cassava Starch of Tanzania Corporation bahati mbaya sana walipata changamoto ya mtaji na hivi sasa wana administration order ya Mahakama ya Biashara Management wameamua kukichukua kiwanda kile na wanatafuta wawekezaji. Wameshakuja wawekezaji kutoka Japan na maeneo mengine na sisi kama Wizara tunaendelea kuwasaidia kutafuta wawekezaji ili kiwanda kile kifufuliwe na kiwe sehemu ya uchakataji wa muhogo ya wakulima wa Mkoa wa Mtwara, Mkoa wa Lindi na Mikoa yote ya Kusini. Nakushukuru sana. (Makofi)