Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwanaisha Ng'anzi Ulenge
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaboresha kadi ya kliniki ya Watoto chini ya miaka mitano ili kusaidia ufuatiliaji wa wingi wa damu?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba moja, upungufu wa damu unaotokana na kukosekana madini chuma unatajwa kuwa chanzo kikuu cha udumavu wa kimo na akili nchini, tatizo ambalo linapelekea Taifa kuwa na watu wasioweza kubuni na wasioweza kujifunza. Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kutatua changamoto hii kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, tafiti zinaonesha kwamba asilimia 47 ya wanawake walio katika umri wa kubeba ujauzito wana tatizo la upungufu wa damu na asilimia 57 kwa wanawake wajazito mtawalia. Sasa ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wasichana wanakuwa na damu sahihi ili kuandaliwa kuwa kinamama wenye afya imara na uwezo wa kuhimili kubeba ujauzito? (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Engineer Ulenge, kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia afya ya watoto na mama na nimeona jinsi anavyoshirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Tanga katika kufuatilia mambo hayo katika Wilaya za Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu maswali yake mawili ambayo kimsingi kwa kweli ni kama swali moja limetenganishwa. Ninachoweza kusema, kwanza Rais wetu Dokta Samia Suluhu Hassan alishazindua Mkakati wa Lishe wa Taifa na kama mnakumbuka aliwasainisha Wakuu wa Mikoa yote kwa ajili ya masuala ya lishe na lishe hiyo sio kwa ajili ya watoto ni kwa ajili ya kila mtu na ambayo kinamama ni sehemu ya wanaotakiwa kufanya hivyo. Maana yake tukizingatia taratibu za lishe hatutakutana na mambo kama haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwamba wakinamama sasa ambao wamefika umri ambao ni wa kubeba mimba na ambao wanajitayarisha, tunafikiri Waheshimiwa Wabunge Mtusaidie kwamba suala la kubeba mimba lisiwe suala la dharura. Kama unataka kubeba mimba, basi unahitajika kujitayarisha na tunashauri waweze kuchukua folic acid. Tunawashauri watumie vidonge vya folic acid na mambo mengine, vitamin kimsingi ukijitayarisha namna hiyo ukibeba mimba hutakuna na upungufu wa damu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia amesema issue ya kimo, uzito na mambo mengine. Ni kweli kwamba suala hili linasababisha pia udumavu wa akili na inatuletea hasara kubwa kwa sababu lina uhusiano na maendeleo yetu, kwamba tusipozingatia haya tunaenda kuwa na kizazi ambacho hakiwezi ku - compete kwenye soko la ajira hakiwezi kuwa innovative na ndiyo maana unaweza kushangaa Tanzania tuna profesa mzuri wa uchumi anakuelezea kupata hela lakini yeye mwenyewe hana hela hayo ndiyo matatizo yanayotokana na mambo kama haya. Ahsante. (Makofi)
Name
Zaytun Seif Swai
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaboresha kadi ya kliniki ya Watoto chini ya miaka mitano ili kusaidia ufuatiliaji wa wingi wa damu?
Supplementary Question 2
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Zaidi ya asilimia 25 ya kinamama ambao wamekwisha jifungua tayari wana upungufu mkubwa wa damu na hivyo kusababisha kuongezeka kwa idadi kubwa ya kinamama waliokwisha jifungua tayari.
Je, Serikali haioni haja sasa ya kuanzisha program maalum ya kuwafuatilia kinamama hawa na kuwasaidia ili kupunguza idadi ya vifo hivi? (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana naye kwamba wakinamama hawa wanapojifungua wanatakiwa kufatiliwa. Ndiyo maana utaona kinamama wakishajifungua kwanza anaenda kliniki akiwa mjamzito, afya yake inafuatiliwa mpaka anapojifungua lakini anakuwa anaenda kliniki na mtoto wakati wote. Kwa hiyo, tutaenda kuendelea kusisitiza kwamba wanapokuja sio tu kumwangalia mtoto na afya ya kinamama iendelee kufatilliwa lakini pia niwaombe hili ni suala la kijamii naendelea kusisitiza Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Kila mtu, suala la lishe na huduma ya mama na mtoto iwe ni ajenda yetu ya kudumu, ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved