Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Primary Question
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji Mwakijembe pamoja na bwawa la kukinga maji?
Supplementary Question 1
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Skimu ya Mwakijembe wananchi wamekuwa wanasubiri kwa takriban miaka 14 sasa. Na kwa kuwa Bunge hili lilipitisha fedha mwaka huu kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu.
Je, Waziri yuko tayari kwenda kusimamia jambo hili ili upembuzi huo na usanifu ukamilike ndani ya mwaka huu tuliotengea fedha na mwaka ujao wa fedha kazi hii ya ujenzi iweze kuanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili skimu hii ilitumia zaidi ya bilioni moja na milioni mia mbili, fedha ambazo ni kama zilipotea kwa sababu skimu haijaweza kufanya kazi.
Je, Wizara iko tayari kwenda kuangalia kwa kina design itakayofanyika ili design hiyo ihusishe ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji na ujenzi wa mifereji ili skimu iweze kutumika kwa uhakika?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula Mbunge Mkinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikiri Mheshimiwa Mbunge amekuwa mfatiliaj mzuri wa jambo hili; na ni kweli skimu hii imekaa muda mrefu. Kulikuwa na changamoto nyingi na hasa kutokana na kwamba katika miaka mingi iliyopita tume yetu haikuwa na uwezo mzuri sana ya kuweza kuisimamia miradi hii mikubwa. Hata hivyo tumefanya mabadiliko makubwa ambapo hivi sasa tumeshamwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuhakikisha ya kwamba wanaipa kipaumbele skimu hii. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili changamoto zilizokuwa zinajitokeza katika miradi iliyopita zisiweze kujirudia, na ikiwemo hoja ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema, ya ujenzi wa mabwawa ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wa mwaka mzima na wakulima wa eneo hilo waweze kufanya kilimo kwa mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwahidi Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tutasimamia kwa ukaribu kabisa kazi hizi zifanyike mapema ili basi tutenge fedha kwa ajili ya ujenzi na wananchi waweze kunufaika na mradi huu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved