Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Felista Deogratius Njau
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuainisha nchi ambazo fursa za biashara na uwekezaji zinaweza kuiletea nchi yetu mapato na kupandisha pato la Taifa zinapatikana?
Supplementary Question 1
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri aliyoyatoa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya diplomasia ya uchumi kwa wananchi ambao ndiyo wadau wakubwa wa dhana hii ikilinganishwa na sasa inafahamika Kitaifa zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; tumeona vyombo vingi vya habari na waandishi wa habari wakiwa nje ya nchi wakiripoti matukio hasi tofauti na fursa zilizoko Tanzania na zinazopatikana nje.
Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha waandishi wa habari walioko nje ya nchi wanatangaza nchi yetu na fursa zilizopo? (Makofi)
Name
Amber. Mbarouk Nassor Mbarouk
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza katika kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ambayo imeweka msisitizo zaidi katika dhana ya diplomasia ya uchumi, Wizara imeendelea kutoa elimu kwa wananchi katika kuelezea fursa mbalimbali zinazopatikana nje ya nchi kupitia makongamano na vyombo vya habari, lakini pia na mitandao ya kijamii. Pia katika maonesho mbalimbali Wizara imekuwa ikitoa hiyo elimu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, Wizara yetu au Serikali inachukua mkakati gani kwa ujumla kwa waandishi wa habari ambao wanapotosha hizi habari nje ya nchi. Kwanza ni kwamba balozi zetu zimekuwa very active mara zinapotokea taarifa hasi, basi mara moja wanashirikiana na vyombo vya habari vya nje katika kuhakikisha kwamba habari zinazotolewa ni za uhakika, ahsante sana.
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri sana aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu niongezee kidogo kwamba kuhusu mkakati wa kutoa elimu ya diplomasia ya uchumi.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu jana wakati Kamati yetu ikitoa taarifa na kama ilivyoelekezwa pia na Kamati, tulieleza kwamba tunaandaa mpango mkakati wa kitaifa wa kutekeleza diplomasia ya uchumi na katika mpango huo, moja ya kitu kitakachojumuishwa ni mpango wa kutoa elimu kwa umma. Kwa hiyo, tutatumia mbinu mbalimbali kuboresha utoaji wa elimu ya umma pamoja na yale tunayoyafanya sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo ni kuhusu tunafanya nini kushirikisha hivi vyombo vinavyotoa elimu hasi kuhusu Tanzania. Tunalifahamu hilo pamoja na hayo yanayofanyika, tayari tumeanza mazungumzo na vile vyombo vya nje hususani vile vinavyoongea Kiswahili kwa sababu sasa hivi tunakuza pia Kiswahili kuwaomba pia wadau wetu.
Mheshimiwa Spika, juzi nimekutana na Idhaa ya Kiswahili ya Uturuki ambao wamefungua idhaa ya kiswahili na moja ya kitu nilichowaomba na mtaona ni kwamba sasa watusaidie kutoa elimu chanya na taarifa chanya kuhusu Taifa letu hususan vivutio tulivyonavyo, fursa tulizonazo na waachane na kutoa elimu hasi. Wao wamekubali kwamba watatusaidia kushirikiana na idhaa nyingine, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved