Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hassan Seleman Mtenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Primary Question
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itasaidia vikundi vya Uvuvi katika Jimbo la Mtwara Mjini?
Supplementary Question 1
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa kunipa majibu yake mazuri sana ambayo nimeyapokea.
Mhshimiwa Spika, Jimbo la Mtwara Mjini ndiyo Jimbo ambalo linazungukwa na bahari. Kwa namna moja au nyingine, vijana wengi wa Mtwara Mjini shughuli zao zinahusika kwenye bahari: Je, ni lini Serikali itanihakikishia kwenye vikundi zaidi ya 30 ambavyo tuliahidiwa kwamba vitapata vitendea kazi, nyavu na vitu vingine, vitasaidiwa? Nipate majibu.
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Tunazungumzia bahari kama bahari: Ni lini Serikali itatuletea meli ya uvuvi ili vijana hawa waweze kupata ajira na samaki ambao wanapotea kwa njia bahari tuweze kunufaika sasa Tanzania kama nchi? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Abdallah Hamis Ulega
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwanza naomba radhi kwa kutokupata majibu haya kwa ufasaha katika meza yako. Naomba nikuahidi kwamba tutafanya marekebisho ya utaratibu huu usirejee tena.
Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini kwanza kwa kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya hasa ile niliyotangulia kuijibu katika jibu la msingi la kuwavuta wawekezaji na kukubali kuwasaidia wana- Mtwara.
Mheshimiwa Spika, kuhusu tutawasaidiaje vijana katika vikundi hivi 30 alivyovitaja waweze kununua nyavu na injini; matarajio yetu katika bajeti inayokuja ya 2022/2023, tunao utaratibu mzuri ambao tutakaposoma bajeti yetu, nataka niwaahidi Waheshimiwa Wabunge wengi, wataona matumaini makubwa ambayo yataenda kujibu swali hili la Mheshimiwa Mtenga. Kwa hiyo, ni matarajio yetu katika mwaka ujao wa fedha, viko vikundi vya vijana vitakavyopata fursa ya kwenda kupata mikopo nafuu ambapo wataweza kununua nyavu na injini.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni juu ya ununuzi wa meli ambazo zitatoa pia ajira kwa vijana. Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ina mkakati mzuri wa kwanza kwa kujenga Bandari ya Uvuvi. Bandari ambayo itajengwa katika Mji wa Kilwa Masoko. Vilevile tunayo bajeti ya kwenda kununua meli za uvuvi zipatazo nne. Meli hizi zitakwenda kuajiri vijana wa Kitanzania wakiwemo vijana kutoka katika Jimbo la Mheshimiwa Hassan Mtenga, kwa maana ya pale Mtwara Mikindani. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Asya Mwadini Mohammed
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itasaidia vikundi vya Uvuvi katika Jimbo la Mtwara Mjini?
Supplementary Question 2
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa ajali nyingi za wavuvi zinazotokea baharini husababishwa na utabiri wa hali ya hewa: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia taarifa za dharura wavuvi wetu kabla ya kuingia baharini? (Makofi)
Name
Abdallah Hamis Ulega
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwadini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni jema na zuri, tumekwishalianza. Kupitia Taasisi ya yetu ya Utafiti ya TAFIRI tumetengeneza programu maalum ya kuwasaidia wavuvi, inayoweza kuwajulisha juu ya makundi ya samaki mahali yalipo. Pia programu hii itaenda mbele, itawasaidia kwenye kufafanua pia na hali ya hewa. Kwa hiyo, ni jambo ambalo tunaendelea nalo hivi sasa na tunalieneza ikiwa ni pamoja na elimu yake ili liweze kuwafaidisha wavuvi wetu.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved