Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Primary Question

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mkoa wa Rukwa unalima zao la maharage ya soya lenye uhitaji mkubwa zaidi duniani?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, maharage ya soya niliyokuwa namaanisha ni maharage ambayo yanatumika kukamua mafuta ya kula, lakini katika majibu ambayo yametolewa na Serikali naamini wanamaanisha maharage ya kula kama mboga.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na majibu hayo, lipo tatizo kubwa sana la upatikanaji wa mbegu za maharage ya soya ambayo yanatumika kwa ajili ya kukamua mafuta. Utakubaliana na mimi kwamba sisi kama Taifa tumepata soko kupeleka maharage haya China.

Swali langu; je, Serikali inafanya mpango gani mahususi wa kuhakikisha kwamba mbegu hizi zinapatikana kwa ajili ya wananchi wa Mikoa ya Rukwa, Ruvuma na mingine yote Tanzania ili tuweze kujitosheleza katika kilimo cha mafuta? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni ukweli usiopingika kwamba kuna formular ya synergy, kwamba moja kujumlisha moja ni tatu na siyo mbili, kwa sababu soya meal inayopatikana ni chakula kizuri sana kwa ajili ya mifugo ikimaanisha ng’ombe, samaki na kuku.

Je, siyo wakati mwafaka kwa Serikali, kwa sababu Wizara ya Mifugo bado bajeti yake haijaja ikahakikisha kwamba ina-inject kiasi cha fedha ili mbegu bora zipatikane ili wakulima na wafugaji wetu wasihangaike ili wawe na uhakika wa chakula kwa ajili ya mifugo? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kandege kwa ujumla wake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli moja kati ya changamoto kubwa tuliyonayo hivi sasa ni upatikanaji wa mbegu bora za soya na Serikali imeanza kuchukua hatua na hatua za kwanza ambazo tumezichukua ni kwa kushirikiana na Taasisi za TOSCI pamoja na ASA kuruhusu uingizaji wa mbegu kutoka nchi za karibu za Malawi na Zambia ili tuweze kufanya seed multiplication na lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunasambaza mbegu hizi kwa wakulima wengi zaidi na zipatikane kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa kunayo changamoto hiyo kubwa, lakini TOSCI na ASA wameshakaa chini na kukubaliana na uingizaji wa mbegu hizi katika hatua ya awali na lengo letu kubwa ni kufanya wananchi wengi zaidi waweze kuzipata kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli liko soko kubwa sana la mahitaji ya soya beans duniani na hasa kule nchini China, mahitaji ni zaidi ya metric tons milioni 100, na kama nchi tumejiandaa pia kulifikia soko hilo. Na katika maeneo ambayo tutayapa kipaumbele ni maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja na hivi sasa Mkurugenzi Mkuu wa ASA yuko njiani anaelekea...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kwa kifupi.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: ...anaelekea kwenda katika Mikoa ya Rukwa na Katavi kwa ajili ya kupata mashamba mengine makubwa kwa ajili ya uzalishaji mbegu ambayo yatakidhi mahitaji ya maeneo husika.

Name

Zaytun Seif Swai

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mkoa wa Rukwa unalima zao la maharage ya soya lenye uhitaji mkubwa zaidi duniani?

Supplementary Question 2

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha wanafanya vizuri sana kwenye zao la vitunguu hapa nchini na hata Afrika Mashariki; je, Wizara ina mkakati gani wa kuwasaidia wakulima hawa ili waweze kuongeza tija na pia kupata masoko ya uhakika? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mikakati tuliyonayo hivi sasa ni kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanalima kwa tija na ili waweze kuyafikia masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi; na kwa kuanzia tumeanza kuwapa maelekezo Maafisa Ugani kwa mazao mahususi ikiwemo vitunguu ili kuwasaidia wakulima waweze kuzalisha kwa tija.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mkoa wa Rukwa unalima zao la maharage ya soya lenye uhitaji mkubwa zaidi duniani?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Njombe na Rukwa ilikuwa inajulikana kama The Big Four kwa kilimo cha mahindi, lakini wakulima wengi sasa hivi wametetereka sana kutokana na bei kubwa ya pembejeo.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba bei ya pembejeo inapungua ili mikoa hiyo iendelee kulima kilimo kikubwa kabisa cha mahindi?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ambayo Serikali tutaichukua kumpunguzia maumivu ya pembejeo mkulima katika bajeti inayokuja tutaanzisha Mfuko maalum, (Price Stabilization Fund) ambao ikitokea pembejeo zitakwenda juu Serikali itatoa ruzuku ili mkulima asiumie sana katika upatikanaji wa pembejeo.