Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sylivia Francis Sigula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza:- Je, ni lini ujenzi wa madarasa katika Kampasi ya Chuo cha Uvuvi Kibirizi utaanza?
Supplementary Question 1
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Wizara, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; uchumi wa vijana wengi wa Mkoa wa Kigoma unategemea sana uvuvi, na sasa hivi tunashukuru kwa sababu tumeanza usafirishaji wa samaki kutoka ndani kwenda nje. Lakini kumekuwa na changamoto, pamoja na kuwa na hiki chuo bado kuna tatizo kubwa la ubora wa samaki wetu kukidhi kwenye masoko ya nje na ndani na chuo hiki kinatoa kozi moja.
Je, Serikali haioni sasa ni muda mwafaka wa kuongeza kozi ya fish processing, quality assurance and marketing ili tuweze kupata wataalam wengi wa kusimamia ubora wa samaki wetu ili kupunguza hasara kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Waziri yuko tayari kuongozana na mimi au Mbunge wa jimbo husika kwenda katika chuo hiki kuona hizi changamoto yeye mwenyewe? (Makofi)
Name
Mashimba Mashauri Ndaki
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Magharibi
Answer
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua umuhimu wa vijana kuingia katika tasnia hii ya uvuvi hasa vijana wa Mkoa wa Kigoma kwa sababu ya mazingira waliyonayo ya Ziwa Tanganyika. Chuo chetu hiki cha Kibirizi kiko kwenye eneo dogo na sisi kama Wizara tunachukua hatua za makusudi kutafuta eneo lingine kwenye Manispaa hiyo hiyo ya Kigoma ili tuweze kukipanua chuo hiki kiweze kutoa mafunzo zaidi kwa vijana hawa ikiwa ni pamoja na kozi aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la kufika Kigoma ili kuweza kuona mazingira halisi, niko tayari kuambatana naye.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved